1Baadaye Mungu akamjaribu Abrahamu. Akamwambia, “Abrahamu!”
2Kisha Mungu akamwambia, “Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, Isaki umpendaye, uende katika nchi ya Moria. Mtoe huko kama sadaka ya kuteketezwa juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.”
3Abrahamu akaamka asubuhi na mapema siku iliyofuata, akamtayarisha punda wake. Akawachukua watumishi wake wawili pamoja na Isaki mwanawe. Baada ya kuchanja kuni za kutosha kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa, akaondoka kuelekea mahali Mungu alipokuwa amemwambia.
4Siku ya tatu Abrahamu akainua macho, akapaona mahali pale kwa mbali.
5Akawaambia watumishi wake, “Kaeni hapa pamoja na punda, wakati mimi na kijana tunakwenda kule. Tutakwenda kuabudu na kisha tutawarudia.”
6Abrahamu akachukua kuni kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, akamtwika Isaki mwanawe, yeye mwenyewe akachukua moto na kisu. Walipokuwa wakienda pamoja,
7Isaki akanena akamwambia Abrahamu baba yake, “Baba yangu!”
8Abrahamu akajibu, “Mwanangu, Mungu mwenyewe atajipatia mwana-kondoo kwa ajili ya hiyo sadaka ya kuteketezwa.” Nao hawa wawili wakaendelea mbele pamoja.
9Walipofika mahali pale alipokuwa ameambiwa na Mungu, Abrahamu akajenga madhabahu hapo, akaziweka kuni juu yake. Akamfunga Isaki mwanawe na akamlaza kwenye madhabahu, juu ya zile kuni.
10Kisha akanyoosha mkono wake na akachukua kisu ili amchinje mwanawe.
11Lakini malaika wa Bwana akamwita kutoka mbinguni, akamwambia, “Abrahamu! Abrahamu!”
12Akamwambia, “Usimdhuru kijana, wala usimtendee jambo lolote. Sasa ninajua kwamba unamcha Mungu, kwa sababu hukunizuilia mwanao, mwana wako wa pekee.”
13Abrahamu akainua macho yake, akaona kondoo dume amenaswa pembe zake nyuma yake katika kichaka. Akaenda akamchukua huyo kondoo dume, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa badala ya mwanawe.
14Abrahamu akapaita mahali pale Yehova-Yire.22:14 Yehova-Yire maana yake Bwana atatupa. Mpaka siku ya leo inasemekana, “Katika mlima wa Bwana itapatikana.”
15Basi malaika wa Bwana akamwita Abrahamu kutoka mbinguni mara ya pili,
16akasema, “Ninaapa kwa nafsi yangu, asema Bwana, kwamba kwa sababu umefanya jambo hili na hukunizuilia mwanao, mwana wako wa pekee,
17hakika nitakubariki, na nitauzidisha uzao wako kama nyota za angani na kama mchanga ulioko pwani. Wazao wako watamiliki miji ya adui zao,
18na kupitia uzao wako mataifa yote duniani yatabarikiwa, kwa sababu umenitii.”
19Ndipo Abrahamu akawarudia watumishi wake, wakaondoka wakaenda wote pamoja mpaka Beer-Sheba. Abrahamu akaishi huko Beer-Sheba.
20Baada ya muda, Abrahamu akaambiwa, “Milka pia amepata watoto, amemzalia ndugu yako Nahori wana:
21Usi mzaliwa wake wa kwanza, Buzi nduguye, Kemueli (baba wa Aramu),
22Kesedi, Hazo, Pildashi, Yidlafu na Bethueli.”
23Bethueli akamzaa Rebeka. Milka alimzalia Nahori nduguye Abrahamu hao wana wanane.
24Suria wake Nahori aliyeitwa Reuma pia alikuwa na wana: Teba, Gahamu, Tahashi na Maaka.