1Wakati huu Bwana akamrehemu Sara kama alivyokuwa amesema, naye Bwana akamtendea Sara kile alichokuwa ameahidi.
2Sara akapata mimba, akamzalia Abrahamu mwana katika uzee wake, majira yale ya Mungu aliomwahidi.
3Abrahamu akamwita Isaki yule mwana ambaye Sara alimzalia.
4Isaki alipokuwa na umri wa siku nane, Abrahamu akamtahiri, kama Mungu alivyomwamuru.
5Abrahamu alikuwa na miaka 100 wakati Isaki mwanawe alipozaliwa.
6Sara akasema, “Mungu ameniletea kicheko, kila mmoja atakayesikia jambo hili atacheka pamoja nami.”
7Akaongeza kusema, “Nani angemwambia Abrahamu kuwa Sara angenyonyesha watoto? Tena nimemzalia mwana katika uzee wake.”
8Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya. Siku hiyo Isaki alipoachishwa kunyonya, Abrahamu alifanya sherehe kubwa.
9Lakini Sara aliona kuwa mwana ambaye Hagari, Mmisri, aliyemzalia Abrahamu alikuwa anadhihaki,
10Sara akamwambia Abrahamu, “Mwondoe mwanamke huyo mtumwa pamoja na mwanawe, kwa kuwa mwana wa mwanamke mtumwa kamwe hatarithi pamoja na mwanangu Isaki.”
11Jambo hili lilimhuzunisha sana Abrahamu kwa sababu lilimhusu mwanawe.
12Lakini Mungu akamwambia, “Usihuzunike hivyo kwa sababu ya kijana na mtumishi wako wa kike. Sikiliza lolote Sara analokuambia, kwa sababu uzao wako utahesabiwa kupitia kwake Isaki.
13Nitamfanya huyu mwana wa mtumishi wako wa kike kuwa taifa pia, kwa sababu naye ni uzao wako.”
14Kesho yake asubuhi na mapema, Abrahamu akachukua chakula na kiriba cha maji, akampa Hagari. Akaviweka mabegani mwa Hagari, akamwondoa pamoja na kijana. Hagari akashika njia, akatangatanga katika jangwa la Beer-Sheba.
15Maji yalipokwisha kwenye kiriba, akamwacha kijana chini ya mojawapo ya vichaka.
16Kisha akajiendea zake akaketi karibu, umbali wa kutupa mshale, akawaza, “Siwezi kumwangalia kijana akifa.” Ikawa alipokuwa ameketi pale karibu, akaanza kulia kwa huzuni.
17Mungu akamsikia kijana akilia, malaika wa Mungu akamwita Hagari kutoka mbinguni na kumwambia, “Kuna nini Hagari? Usiogope, Mungu amesikia kijana analia akiwa amelala pale.
18Mwinue kijana na umshike mkono, kwa maana nitamfanya kuwa taifa kubwa.”
19Ndipo Mungu akamfumbua Hagari macho yake naye akaona kisima cha maji. Hivyo akaenda akajaza kiriba maji na kumpa kijana anywe.
20Mungu akawa pamoja na huyu kijana alipokuwa akiendelea kukua. Aliishi jangwani na akawa mpiga upinde.
21Alipokuwa akiishi katika Jangwa la Parani, mama yake akampatia mke kutoka Misri.
22Wakati huo Abimeleki na Fikoli mkuu wa majeshi yake wakamwambia Abrahamu, “Mungu yu pamoja nawe katika kila kitu unachofanya.
23Sasa niapie hapa mbele za Mungu kwamba hutanitenda hila mimi, watoto wangu wala wazao wangu. Nitendee mimi na nchi ambayo unaishi kama mgeni wema ule ule ambao nimekutendea.”
24Abrahamu akasema, “Ninaapa hivyo.”
25Ndipo Abrahamu akalalamika kwa Abimeleki kuhusu kisima cha maji ambacho watumishi wa Abimeleki walikuwa wamekinyangʼanya.
26Lakini Abimeleki akasema, “Sijui ni nani ambaye amefanya hili. Hukuniambia, leo tu ndipo ninasikia habari zake.”
27Hivyo Abrahamu akaleta kondoo na ngʼombe, akampa Abimeleki, nao watu hawa wawili wakafanya mapatano.
28Abrahamu akatenga kondoo wa kike saba kutoka kwenye kundi,
29Abimeleki akamuuliza Abrahamu, “Ni nini maana ya hawa kondoo wa kike saba uliowatenga peke yao?”
30Abrahamu akamjibu, “Upokee hawa kondoo wa kike saba kutoka mkononi mwangu kama ushahidi kuwa nilichimba kisima hiki.”
31Hivyo mahali pale pakaitwa Beer-Sheba, kwa sababu watu wawili waliapiana hapo.
32Baada ya mapatano kufanyika huko Beer-Sheba, Abimeleki na Fikoli mkuu wa majeshi yake wakarudi katika nchi ya Wafilisti.
33Abrahamu akapanda mti wa mkwaju huko Beer-Sheba, na hapo akaliitia jina la Bwana, Mungu wa milele.
34Naye Abrahamu akakaa katika nchi ya Wafilisti kwa muda mrefu.