1Wakati huo dunia yote ilikuwa na lugha moja na msemo mmoja.
2Watu walipoelekea upande wa mashariki, wakafika kwenye tambarare katika nchi ya Shinari11:2 Shinari ndio Babeli. nao wakaishi huko.
3Wakasemezana wao kwa wao, “Njooni, tufyatue matofali na tuyachome vizuri kwa moto.” Walitumia matofali badala ya mawe, na lami kwa ajili ya kushikamanishia hayo matofali.
4Ndipo wakasema, “Njooni, tujijengee mji wenye mnara ambao utafika hadi mbinguni, ili tujipatie jina tusije tukatawanyika usoni pa dunia yote.”
5Lakini Bwana akashuka ili auone mji na mnara ambao wanadamu waliokuwa wanaujenga.
6Bwana akasema, “Ikiwa kama taifa moja wanaozungumza lugha moja wameanza kufanya hili, basi hakuna lolote watakalopanga kufanya ambalo halitawezekana kwao.
7Njooni, tushuke tuvuruge lugha yao ili wasielewane wao kwa wao.”
8Hivyo Bwana akawatawanya kutoka mahali pale kwenda katika dunia yote, nao wakaacha kuujenga huo mji.
9Ndiyo maana pakaitwa Babeli, kwa sababu hapo ndipo Bwana alipoivuruga lugha ya dunia nzima. Kutoka hapo Bwana akawatawanya katika uso wa dunia yote.
10Hivi ndivyo vizazi vya Shemu.
11Baada ya kumzaa Arfaksadi, Shemu aliishi miaka 500, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
12Wakati Arfaksadi alipokuwa na miaka thelathini na mitano, akamzaa Shela.
13Baada ya Arfaksadi kumzaa Shela, aliishi miaka 403, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
14Shela alipokuwa na miaka thelathini, akamzaa Eberi.
15Shela baada ya kumzaa Eberi, aliishi miaka 403, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
16Eberi alipokuwa na miaka thelathini na minne, akamzaa Pelegi.
17Baada ya Eberi kumzaa Pelegi, aliishi miaka 430, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
18Pelegi alipokuwa na miaka thelathini, akamzaa Reu.
19Baada ya Pelegi kumzaa Reu, aliishi miaka 209, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
20Reu alipokuwa na miaka thelathini na miwili, akamzaa Serugi.
21Baada ya Reu kumzaa Serugi, aliishi miaka 207, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
22Serugi alipokuwa na miaka thelathini, akamzaa Nahori.
23Baada ya Serugi kumzaa Nahori, aliishi miaka 200, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
24Nahori alipokuwa na miaka ishirini na tisa, akamzaa Tera.
25Baada ya Nahori kumzaa Tera, aliishi miaka 119, akazaa watoto wengine wa kiume na wa kike.
26Tera alipokuwa na miaka sabini, akamzaa Abramu, Nahori na Harani.
27Hawa ndio wazao wa Tera.
28Tera alipokuwa bado hai, Harani akafa huko Uru ya Wakaldayo, nchi alimozaliwa.
29Abramu na Nahori walioa. Mke wa Abramu aliitwa Sarai, na mke wa Nahori aliitwa Milka; Milka na Iska walikuwa watoto wa Harani.
30Sarai alikuwa tasa, hakuwa na watoto.
31Tera akamchukua Abramu mwanawe, Loti mwana wa Harani mwanawe, na Sarai mkwewe, mke wa Abramu mwanawe, wakatoka kwa pamoja katika Uru ya Wakaldayo kwenda nchi ya Kanaani. Lakini walipofika Harani, wakaishi huko.
32Tera alikufa huko Harani akiwa na miaka 205.