We Believe JesusFé, Esperança e Nova Vida

Kutoka 16

Biblica® Toleo Wazi la Neno: Biblia Takatifu™ · suaíli

← Kutoka 15 Kutoka Kutoka 17 →

1Jumuiya yote ya Kiisraeli ikaondoka Elimu, wakafika Jangwa la Sini, lililokuwa kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka Misri.

2Huko jangwani hiyo jumuiya yote wakawanungʼunikia Mose na Aroni.

3Waisraeli wakawaambia, “Laiti tungelikufa kwa mkono wa Bwana huko Misri! Huko tuliketi tukizunguka masufuria ya nyama na tukala vyakula tulivyovitaka, lakini ninyi mmetuleta huku jangwani ili mpate kuua mkutano huu wote kwa njaa.”

4Kisha Bwana akamwambia Mose, “Nitanyesha mikate kutoka mbinguni kwa ajili yenu. Watu watatoka kila siku na kukusanya kitakachowatosha kwa siku ile, kwa njia hii, nitawajaribu nione kama watafuata maelekezo yangu.

5Siku ya sita watatayarisha kile waletacho ndani, nacho kitakuwa mara mbili kuliko ya kile walichokusanya kila siku.”

6Kwa hiyo Mose na Aroni wakawaambia Waisraeli wote, “Jioni mtajua kwamba Bwana ndiye aliwatoa Misri,

7kisha asubuhi mtauona utukufu wa Bwana, kwa sababu amesikia manungʼuniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani hata mtunungʼunikie?”

8Pia Mose akasema, “Mtajua kuwa alikuwa Bwana wakati atakapowapa nyama mle ifikapo jioni na mikate yote mtakayohitaji asubuhi kwa sababu amesikia manungʼuniko yenu dhidi yake. Sisi ni nani? Hamnungʼuniki dhidi yetu, bali dhidi ya Bwana.”

9Kisha Mose akamwambia Aroni, “Iambie jumuiya yote ya Waisraeli kwamba, ‘Mje mbele zake Bwana, kwa maana amesikia manungʼuniko yenu.’ ”

10Aroni alipokuwa akizungumza na jumuiya yote ya Waisraeli, wakatazama kuelekea jangwani, na huko wakaona utukufu wa Bwana ukitokeza katika wingu.

11Bwana akamwambia Mose,

12“Nimesikia manungʼuniko ya Waisraeli. Waambie, ‘Jioni mtakula nyama, na asubuhi mtashiba mikate. Ndipo mtajua ya kwamba Mimi ndimi Bwana Mungu wenu.’ ”

13Jioni ile kware wakaja wakaifunika kambi na asubuhi kulikuwa na tabaka la umande kuzunguka kambi.

14Wakati umande ulipoondoka, vipande vidogo vidogo kama theluji vilionekana juu ya uso wa jangwa.

15Waisraeli walipoona, wakaambiana, “Hiki ni nini?” Kwa kuwa hawakujua kilikuwa kitu gani.

16Hivi ndivyo Bwana alivyoamuru: ‘Kila mmoja akusanye kiasi anachohitaji. Chukueni pishi16:16 Pishi ni kipimo cha ujazo, kwa Kiebrania ni omeri, ambacho ni sawa na kilo mbili. moja kwa kila mtu mliye naye katika hema yenu.’ ”

17Waisraeli wakafanya kama walivyoambiwa, baadhi yao wakakusanya zaidi, wengine pungufu.

18Nao walipopima katika pishi, yule aliyekusanya zaidi hakuwa na ziada, wala aliyekusanya kidogo hakupungukiwa. Kila mmoja alikusanya kiasi alichohitaji.

19Kisha Mose akawaambia, “Mtu yeyote asibakize chochote mpaka asubuhi.”

20Hata hivyo, wengine hawakuzingatia aliyosema Mose, wakahifadhi kiasi fulani mpaka asubuhi, lakini kile alichohifadhi kikajaa mabuu na kuanza kunuka. Kwa hiyo Mose akawakasirikia.

21Kila asubuhi, kila mmoja alikusanya kiasi alichohitaji na jua lilipokuwa kali, iliyeyuka.

22Siku ya sita, wakakusanya mara mbili, kiasi cha pishi mbili kwa kila mtu, nao viongozi wa jumuiya wakaja kumwarifu Mose.

23Mose akawaambia, “Hivi ndivyo alivyoagiza Bwana: ‘Kesho itakuwa siku ya mapumziko, Sabato takatifu kwa Bwana. Kwa hiyo okeni kile mnachotaka kuoka na mchemshe kile mnachotaka kuchemsha. Hifadhini chochote kinachobaki na mkiweke mpaka asubuhi.’ ”

24Kwa hiyo wakavihifadhi mpaka asubuhi, kama Mose alivyoagiza, na havikunuka wala kuwa na mabuu.

25Mose akawaambia, “Kuleni leo, kwa sababu leo ni Sabato kwa Bwana. Hamtapata chochote juu ya nchi leo.

26Kwa siku sita mtakusanya, lakini siku ya saba, yaani Sabato, hakutakuwepo chochote.”

27Hata hivyo, baadhi ya watu wakatoka kwenda kukusanya siku ya saba, lakini hawakupata chochote.

28Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Je, mtaacha kushika maagizo na maelekezo yangu mpaka lini?

29Fahamuni kuwa Bwana amewapa ninyi Sabato, ndiyo sababu katika siku ya sita amewapa mikate ya siku mbili. Kila mmoja inampasa kukaa pale alipo katika siku ya saba. Hata mmoja haruhusiwi kutoka.”

30Kwa hiyo watu wakapumzika siku ya saba.

31Watu wa Israeli wakaita ile mikate mana16:31 Mana maana yake ni mkate kutoka mbinguni. Ilikuwa myeupe kama mbegu za mtama na ladha yake ilikuwa kama mkate mwembamba uliotengenezwa kwa asali.

32Mose akasema, “Hivi ndivyo alivyoagiza Bwana: ‘Chukueni pishi ya mana na kuhifadhi kwa ajili ya vizazi vijavyo ili vione mikate niliyowapa mle jangwani nilipowatoa katika nchi ya Misri.’ ”

33Kwa hiyo Mose akamwambia Aroni, “Chukua gudulia na uweke pishi moja ya mana ndani yake. Kisha uweke mbele za Bwana ili kihifadhiwe kwa ajili ya vizazi vijavyo.”

34Kama Bwana alivyomwagiza Mose, hatimaye Aroni alikuja kuihifadhi ndani ya Sanduku la Ushuhuda.

35Waisraeli wakala mana kwa miaka arobaini, mpaka walipofika katika nchi iliyokaliwa na watu; walikula mana hadi walipofika mpakani mwa Kanaani.

36(Pishi moja ni sehemu ya kumi ya kipimo cha efa.16:36 Efa moja ni sawa na kilo 22.)

← Kutoka 15 Kutoka Kutoka 17 →