We Believe JesusFé, Esperança e Nova Vida

1 Wathesalonike 5

Biblica® Toleo Wazi la Neno: Biblia Takatifu™ · suaíli

← 1 Wathesalonike 4 1 Wathesalonike

1Basi, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira hatuna haja ya kuwaandikia,

2kwa kuwa mnajua vyema kwamba siku ya Bwana itakuja kama mwizi ajapo usiku.

3Wakati watu wanaposema, “Kuna amani na salama,” maangamizi huwajia ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwanamke mwenye mimba; nao hakika hawatatoroka.

4Bali ninyi, ndugu, hampo gizani hata siku ile iwakute ghafula kama mwizi.

5Ninyi nyote ni wana wa nuru na wana wa mchana. Sisi si wana wa giza wala wa usiku.

6Kwa hiyo basi, tusilale kama watu wengine walalavyo, bali tukeshe na kuwa na kiasi.

7Kwa kuwa wote walalao hulala usiku na wale walewao hulewa usiku.

8Lakini kwa kuwa sisi ni wana wa mchana, basi tuwe na kiasi, tukijivika imani na upendo kama dirii kifuani na tumaini letu la wokovu kama chapeo.

9Kwa maana Mungu hakutuita ili tupate ghadhabu bali tupate wokovu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.

10Yeye alikufa kwa ajili yetu ili hata kama tuko macho au tumelala, tupate kuishi pamoja naye.

11Kwa hiyo farijianeni na kujengana, kama vile mnavyofanya sasa.

12Sasa tunawaomba, ndugu, waheshimuni wale wanaofanya kazi kwa bidii miongoni mwenu, wale ambao wana mamlaka juu yenu katika Bwana na ambao wanawaonya.

13Waheshimuni sana katika upendo kwa ajili ya kazi zao. Ishini kwa amani ninyi kwa ninyi.

14Nasi twawasihi, ndugu, waonyeni walio wavivu, watieni moyo waoga, wasaidieni wanyonge na kuwavumilia watu wote.

15Angalieni kuwa mtu asimlipe mwenzake maovu kwa maovu, bali siku zote tafuteni kutendeana mema ninyi kwa ninyi na kwa watu wote.

16Furahini siku zote;

17ombeni bila kukoma;

18shukuruni kwa kila jambo, kwa maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu kwa ajili yenu katika Kristo Yesu.

19Msiuzime moto wa Roho Mtakatifu;

20msiyadharau maneno ya unabii.

21Jaribuni kila kitu. Yashikeni yaliyo mema.

22Jiepusheni na uovu wa kila namna.

23Mungu mwenyewe, Mungu wa amani, awatakase ninyi kabisa. Nanyi mhifadhiwe roho zenu, nafsi zenu na miili yenu, bila kuwa na lawama katika Bwana wetu Yesu Kristo.

24Yeye aliyewaita ni mwaminifu naye atafanya hayo.

25Ndugu, tuombeeni.

26Wasalimuni ndugu wote kwa busu takatifu.

27Nawaagizeni mbele za Bwana mhakikishe kuwa ndugu wote wanasomewa barua hii.

28Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi. Amen.

← 1 Wathesalonike 4 1 Wathesalonike