We Believe JesusFé, Esperança e Nova Vida

1 Wathesalonike 4

Biblica® Toleo Wazi la Neno: Biblia Takatifu™ · suaíli

← 1 Wathesalonike 3 1 Wathesalonike 1 Wathesalonike 5 →

1Hatimaye, ndugu, tuliwaomba na kuwasihi katika Bwana Yesu kwamba, kama mlivyojifunza kutoka kwetu jinsi iwapasavyo kuishi ili kumpendeza Mungu, kama vile mnavyoishi, imewapasa mzidi sana kufanya hivyo.

2Kwa kuwa mnajua ni maagizo gani tuliyowapa kwa mamlaka ya Bwana Yesu.

3Mapenzi ya Mungu ni kwamba ninyi mtakaswe, ili kwamba mjiepushe na zinaa,

4ili kwamba kila mmoja wenu ajifunze kuutawala mwili wake mwenyewe katika utakatifu na heshima,

5si kwa tamaa mbaya kama watu wa Mataifa wasiomjua Mungu.

6Katika jambo hili mtu asimkosee ndugu yake wala kumlaghai. Kwa kuwa Bwana ni mlipiza kisasi katika mambo haya yote, kama vile tulivyokwisha kuwaambia mapema na kuwaonya vikali.

7Kwa maana Mungu hakutuitia uchafu, bali utakatifu.

8Kwa hiyo, mtu yeyote anayekataa mafundisho haya hamkatai mwanadamu, bali anamkataa Mungu anayewapa ninyi Roho wake Mtakatifu.

9Sasa kuhusu upendo wa ndugu hamna haja mtu yeyote kuwaandikia, kwa maana ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana.

10Nanyi kwa kweli mnawapenda ndugu wote katika Makedonia nzima. Lakini ndugu, tunawasihi mzidi sana kuwapenda.

11Jitahidini kuishi maisha ya utulivu, kila mtu akijishughulisha na mambo yake mwenyewe na kufanya kazi kwa mikono yake, kama vile tulivyowaagiza,

12ili maisha yenu ya kila siku yajipatie heshima kutoka kwa watu walio nje, ili msimtegemee mtu yeyote.

13Lakini ndugu, hatutaki mkose kujua kuhusu wale waliolala mauti, ili msihuzunike kama watu wengine wasiokuwa na tumaini.

14Kwa kuwa tunaamini kwamba Yesu alikufa na kufufuka, na kwa hivyo, Mungu kwa njia ya Yesu atawafufua pamoja naye wale waliolala mautini ndani yake.

15Kulingana na neno la Bwana mwenyewe, tunawaambia kwamba sisi ambao bado tuko hai, tuliobaki hadi kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia waliolala mauti.

16Kwa maana Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni, akitoa amri kwa sauti kuu, pamoja na sauti ya malaika mkuu, na sauti ya tarumbeta ya Mungu. Nao waliokufa wakiwa katika Kristo watafufuka kwanza.

17Baada ya hilo sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu ili kumlaki Bwana hewani, hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele.

18Kwa hiyo farijianeni kwa maneno haya.

← 1 Wathesalonike 3 1 Wathesalonike 1 Wathesalonike 5 →