We Believe JesusFé, Esperança e Nova Vida

1 Nyakati 17

Biblica® Toleo Wazi la Neno: Biblia Takatifu™ · suaíli

← 1 Nyakati 16 1 Nyakati 1 Nyakati 18 →

1Baada ya Daudi kuingia rasmi katika jumba lake la kifalme, akamwambia nabii Nathani, “Hebu tazama, mimi ninakaa kwenye nyumba nzuri iliyojengwa kwa mierezi, wakati Sanduku la Agano la Bwana liko ndani ya hema.”

2Nathani akamjibu Daudi, “Lolote ulilo nalo moyoni mwako litende, kwa maana Mungu yu pamoja nawe.”

3Usiku ule neno la Mungu likamjia Nathani, kusema:

4“Nenda ukamwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Wewe hutanijengea mimi nyumba ili nikae humo.

5Mimi sijakaa ndani ya nyumba tangu siku ile niliyowatoa Israeli kutoka Misri mpaka leo. Nimehama kutoka hema moja hadi jingine na kutoka mahali pamoja hadi pengine.

6Je, popote nilipokwenda pamoja na Waisraeli wote, wakati wowote nilimwambia kiongozi yeyote niliyemwagiza kuwachunga watu wangu, kwa nini hujanijengea nyumba ya mierezi?’

7“Sasa basi, mwambie mtumishi wangu Daudi, ‘Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: Nilikuchukua machungani na kutoka kuandama kondoo ili uwatawale watu wangu Israeli.

8Nimekuwa pamoja nawe popote ulipokwenda, nami nimekuondolea mbali adui zako wote mbele yako. Basi nitalifanya jina lako kuwa kuu kama majina ya watu walio wakuu sana duniani.

9Nami nitawapatia watu wangu Israeli mahali na nitawapa ili wawe na mahali pao wenyewe pa kuishi na wasisumbuliwe tena. Watu waovu hawatawaonea tena, kama walivyofanya mwanzoni,

10na ambavyo wamefanya siku zote tangu nilipowachagua viongozi kwa ajili ya watu wangu Israeli. Pia nitawatiisha adui zenu wote.

11Wakati wako utakapokuwa umekwisha, nawe ukawa umekwenda kukaa na baba zako, nitamwinua mzao wako aingie mahali pako kuwa mfalme, mmoja wa wana wako mwenyewe, nami nitaufanya imara ufalme wake.

12Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili yangu, nami nitakifanya imara kiti cha ufalme wake milele.

13Mimi nitakuwa baba yake, naye atakuwa mwanangu. Kamwe sitaondoa upendo wangu kwake, kama nilivyouondoa kwa yeye aliyekutangulia.

14Nitamweka juu ya nyumba yangu na ufalme wangu milele; kiti chake cha enzi nitakifanya imara milele.’ ”

15Nathani akamwarifu Daudi maneno yote ya maono haya.

16Ndipo Mfalme Daudi akaingia ndani, akaketi mbele za Bwana, akasema:

17Kana kwamba hili halitoshi machoni pako, Ee Mungu, umenena pia kuhusu siku zijazo za nyumba ya mtumishi wako. Umeniangalia kama mtu aliyetukuka kuliko watu wote, Ee Bwana Mungu.

18“Daudi aweza kukuambia nini zaidi kuhusu kumheshimu mtumishi wako? Kwa maana wewe unamjua mtumishi wako,

19Ee Bwana Mungu. Kwa ajili ya mtumishi wako, tena sawasawa na mapenzi yako, umefanya jambo hili kubwa sana na kujulisha ahadi hizi zote zilizo kubwa sana.

20“Hakuna aliye kama wewe, Ee Bwana Mungu, wala hakuna Mungu ila wewe, kama vile tulivyosikia kwa masikio yetu wenyewe.

21Naye ni nani aliye kama watu wako Israeli: taifa pekee duniani ambalo Mungu wake alitoka kwenda kulikomboa kwa ajili yake mwenyewe na kujifanyia jina kwa ajili yake mwenyewe, kwa kufanya maajabu makubwa na ya kutisha kwa kuwafukuza mataifa mbele ya watu wako, ambao uliwakomboa kutoka Misri?

22Uliwafanya watu wako Israeli kuwa watu wako wewe mwenyewe milele, nawe, Ee Bwana Mungu, umekuwa Mungu wao.

23“Sasa basi, Bwana ahadi uliyoweka kuhusu mtumishi wako na nyumba yake na uithibitishe milele. Fanya kama ulivyoahidi,

24ili ithibitike na jina lako litakuwa kuu milele. Kisha watu watasema, ‘Bwana Mungu Mwenye Nguvu Zote, Mungu aliye juu ya Israeli, ndiye Mungu wa Israeli.’ Nayo nyumba ya mtumishi wako Daudi itafanywa imara mbele zako.

25“Wewe, Mungu wangu, umemfunulia mtumishi wako Daudi kwamba utamjengea yeye nyumba. Hivyo mtumishi wako amekuwa na ujasiri wa kukuomba maombi haya.

26Ee Bwana, wewe ndiwe Mungu! Umemwahidi mtumishi wako mambo haya mazuri.

27Basi imekupendeza kuibariki nyumba ya mtumishi wako, ili idumu milele machoni pako; kwa ajili yako, Ee Bwana, umeibariki, nayo itabarikiwa milele.”

← 1 Nyakati 16 1 Nyakati 1 Nyakati 18 →