We Believe JesusFé, Esperança e Nova Vida

Hesabu 18

Biblica® Toleo Wazi la Neno: Biblia Takatifu™ · suaíli

← Hesabu 17 Hesabu Hesabu 19 →

1Bwana akamwambia Aroni, “Wewe, wanao na jamaa ya baba yako mtawajibika kwa makosa dhidi ya mahali patakatifu, na wewe na wanao peke yenu ndio mtakaowajibika kwa makosa dhidi ya ukuhani.

2Walete Walawi wenzako kutoka kabila la baba zako ili waungane nanyi na kuwasaidia wakati wewe na wanao mnapohudumu mbele ya Hema la Ushuhuda.

3Watawajibika kwenu na watafanya kazi zote za Hema, lakini kamwe wasisogelee vifaa vya patakatifu au madhabahu, la sivyo wao na ninyi mtakufa.

4Watajiunga nanyi na watawajibika kwa utunzaji wa Hema la Kukutania, yaani kazi zote kwenye Hema, wala hakuna mtu mwingine yeyote atakayeweza kusogea karibu hapo mlipo.

5“Mtawajibika katika utunzaji wa mahali patakatifu na madhabahu, ili kwamba ghadhabu isiwaangukie Waisraeli tena.

6Mimi mwenyewe nimewachagua Walawi wenzenu kutoka miongoni mwa Waisraeli kama zawadi kwenu, waliowekwa wakfu kwa Bwana ili kufanya kazi katika Hema la Kukutania.

7Lakini ni wewe tu na wanao mtakaoweza kutumika kama makuhani kuhusiana na kila kitu kwenye madhabahu na ndani ya pazia. Ninawapa utumishi wa ukuhani kama zawadi. Mtu mwingine yeyote atakayekaribia mahali patakatifu ni lazima auawe.”

8Kisha Bwana akamwambia Aroni, “Mimi mwenyewe nimekuweka kuwa mwangalizi wa sadaka zote zitakazotolewa kwangu; matoleo yote matakatifu Waisraeli wanayonipa ninakupa wewe na wanao kama sehemu yenu na fungu lenu la kawaida.

9Mtachukua sehemu ya yale matoleo matakatifu sana ambayo hayateketezwi kwa moto. Kutoka kwa matoleo yote wanayoniletea kama sadaka takatifu sana, ziwe za nafaka, au za dhambi, au za makosa, sehemu ile itakuwa yako na wanao.

10Mtaila kama kitu kilicho kitakatifu sana; kila mwanaume ataila. Ni lazima mtaiheshimu kama takatifu.

11“Hiki pia ni chako: chochote kilichotengwa kutoka kwenye matoleo yote ya sadaka za kuinuliwa za Waisraeli. Ninakupa wewe haya, wana na binti zako kama sehemu yenu ya kawaida. Kila mmoja wa nyumba yako ambaye ni safi kwa taratibu za ibada anaweza kuyala.

12“Ninawapa mafuta ya zeituni yaliyo bora kuliko yote, na divai mpya iliyo bora kuliko zote na nafaka wanazompa Bwana kama malimbuko katika mavuno yao.

13Malimbuko yote ya nchi ambayo wanamletea Bwana yatakuwa yenu. Kila mmoja nyumbani kwako ambaye ni safi kwa taratibu za Ibada anaweza kula.

14“Kila kitu katika Israeli ambacho kimetolewa kwa Bwana ni chenu.

15Kila mzaliwa wa kwanza wa mwanadamu na wa mnyama, ambaye ametolewa kwa Bwana ni wenu. Lakini ni lazima mtamkomboa kila mwana mzaliwa wa kwanza na kila mzaliwa wa kwanza wa kiume wa wanyama wasio safi.

16Watakapokuwa na umri wa mwezi mmoja, ni lazima mtawakomboa kwa bei ya ukombozi iliyowekwa, kwa shekeli tano18:16 Shekeli tano za fedha ni sawa na gramu 55. za fedha, kulingana na shekeli ya mahali patakatifu, yenye uzito wa gera ishirini.18:16 Gera 20 ni sawa na gramu 55.

17“Lakini kamwe usimkomboe mzaliwa wa kwanza wa maksai, kondoo au mbuzi; hawa ni watakatifu. Nyunyizia damu yao juu ya madhabahu na uchome mafuta yao kama sadaka itolewayo kwa moto, harufu nzuri inayompendeza Bwana.

18Nyama zao zitakuwa chakula chenu, kama ilivyokuwa kidari cha kuinuliwa na paja la mguu wa kulia.

19Chochote kitakachotengwa kutoka sadaka takatifu ambazo Waisraeli wanamtolea Bwana, ninakupa wewe, wanao na binti zako kama fungu lenu la kawaida. Ni Agano la milele la chumvi mbele za Bwana kwako na watoto wako.”

20Bwana akamwambia Aroni, “Hutakuwa na urithi wowote katika nchi yao, wala hutakuwa na sehemu miongoni mwao; Mimi ni fungu lako na urithi wako miongoni mwa Waisraeli.

21“Ninawapa Walawi zaka yote katika Israeli kama urithi wao kuwa kama malipo kwa kazi wanayoifanya wakati wanapohudumu katika Hema la Kukutania.

22Kuanzia sasa, kamwe Waisraeli wasisogelee karibu na Hema la Kukutania, la sivyo watabeba matokeo ya dhambi zao, nao watakufa.

23Ni Walawi watakaofanya kazi katika Hema la Kukutania na kubeba wajibu wa makosa dhidi yake. Hili ni agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo. Hawatapokea urithi wowote miongoni mwa Waisraeli.

24Badala yake, ninawapa Walawi zaka zote zinazotolewa na Waisraeli kama sadaka kwa Bwana kuwa urithi wao. Hiyo ndiyo sababu nimesema hivi kuhusu wao: ‘Hawatakuwa na urithi miongoni mwa Waisraeli.’ ”

25Bwana akamwambia Mose,

26“Sema na Walawi na uwaambie: ‘Mtakapopokea zaka kutoka kwa Waisraeli ambayo ninawapa kama urithi wenu kutoka kwao, ni lazima mtoe sehemu ya kumi ya hiyo zaka kama sadaka kwa Bwana, iwe zaka ya hiyo zaka.

27Sadaka yenu itahesabiwa kwenu kama nafaka kutoka sakafu ya kupuria, au divai kutoka kwenye shinikizo la kukamulia zabibu.

28Kwa njia hii, ninyi pia mtatoa sadaka kwa Bwana kutoka zaka zote mtakazopokea kutoka kwa Waisraeli. Kutoka kwenye zaka hizi, ni lazima mtoe sehemu ya Bwana kwa Aroni, kuhani.

29Ni lazima mtoe kama sehemu ya Bwana iliyo nzuri sana tena ile sehemu iliyo takatifu sana kuliko zote ya kile kitu mlichopewa.’

30“Waambie Walawi: ‘Mtakapotoa sehemu zilizo bora sana, itahesabiwa kwenu kama mazao ya sakafu ya kupuria nafaka, au ya shinikizo la kukamulia zabibu.

31Ninyi na watu wa nyumbani mwenu mnaweza kula sehemu iliyobaki mahali popote, kwani ndio ujira wenu kwa ajili ya kazi yenu katika Hema la Kukutania.

32Kwa kutoa sehemu zake zilizo bora sana, hamtakuwa na hatia katika jambo hili; ndipo hamtatia unajisi sadaka takatifu za Waisraeli, nanyi hamtakufa.’ ”

← Hesabu 17 Hesabu Hesabu 19 →