1Wakasafiri kupitia Amfipoli na Apolonia wakafika Thesalonike, ambako kulikuwa na sinagogi la Wayahudi.
2Kama desturi yake, Paulo aliingia ndani ya sinagogi, na kwa muda wa Sabato tatu akawa anahojiana nao kutoka kwenye Maandiko,
3akidhihirisha wazi na kuthibitisha kwamba ilikuwa lazima Kristo17:3 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta. ateswe na afufuke kutoka kwa wafu. Akasema, “Huyu Yesu ninayewaambia habari zake, ndiye Kristo.”
4Baadhi ya Wayahudi wakasadiki, wakaungana na Paulo na Sila, wakiwepo idadi kubwa ya Wayunani waliomcha Mungu na wanawake wengi mashuhuri.
5Lakini Wayahudi ambao hawakuwa wameamini wakawa na wivu, wakawakodi watu waovu kutoka sokoni, wakakutanisha umati wa watu, wakaanzisha ghasia mjini. Wakaenda mbio nyumbani kwa Yasoni wakiwatafuta Paulo na Sila ili kuwaleta nje penye ule umati wa watu.
6Lakini walipowakosa wakamburuta Yasoni na ndugu wengine mbele ya maafisa wa mji, wakipiga kelele: “Watu hawa ni wale walioupindua ulimwengu wamekuja huku,
7naye Yasoni amewakaribisha nyumbani mwake. Hawa wote wanaasi amri za Kaisari wakisema yuko mfalme mwingine aitwaye Yesu.”
8Waliposikia haya, ule umati wa watu na maafisa wa mji wakaongeza ghasia.
9Nao baada ya kuchukua dhamana kwa ajili ya Yasoni na wenzake wakawaacha waende zao.
10Usiku ule ule, wale ndugu walioamini wakawapeleka Paulo na Sila waende zao Beroya. Walipowasili huko wakaenda kwenye sinagogi la Wayahudi.
11Hawa Waberoya walikuwa waungwana zaidi kuliko wale wa Thesalonike, kwa kuwa waliupokea ule ujumbe kwa shauku kubwa na kuyachunguza Maandiko kila siku ili kuona kama yale Paulo aliyosema yalikuwa kweli.
12Wayahudi wengi wakaamini pamoja na wanawake na wanaume wa Kiyunani wa tabaka la juu.
13Lakini wale Wayahudi wa Thesalonike waliposikia kuwa Paulo anahubiri neno la Mungu huko Beroya, wakaenda huko ili kuwashawishi watu na kuwachochea.
14Mara hiyo, wale ndugu wakamsafirisha Paulo hadi pwani, lakini Sila na Timotheo wakabaki Beroya.
15Wale waliomsindikiza Paulo wakaenda naye mpaka Athene, kisha wakarudi Beroya wakiwa na maagizo kutoka kwa Paulo kuhusu Sila na Timotheo kwamba wamfuate upesi iwezekanavyo.
16Paulo alipokuwa akiwasubiri huko Athene, alisumbuka sana moyoni mwake kuona vile mji huo ulivyojaa sanamu.
17Hivyo akahojiana kwenye sinagogi na Wayahudi pamoja na Wayunani waliomcha Mungu, na pia sokoni kila siku na watu aliopatana nao huko.
18Kisha baadhi ya Waepikureo na Wastoiko wenye falsafa wakakutana naye. Baadhi yao wakasema, “Je, huyu mpayukaji anajaribu kusema nini?” Wengine wakasema, “Inaonekana anasema habari za miungu ya kigeni.” Walisema haya kwa sababu Paulo alikuwa anahubiri habari njema kuhusu Yesu na ufufuo wa wafu.
19Hivyo wakamchukua na kumleta kwenye mkutano wa Areopago, walikomwambia, “Je, tunaweza kujua mafundisho haya mapya unayofundisha ni nini?
20Wewe unaleta mambo mapya masikioni mwetu, hivyo tungetaka kujua maana yake ni nini.”
21(Waathene na wageni wote walioishi humo hawakutumia muda wao kufanya chochote kingine isipokuwa kueleza au kusikia mambo mapya).
22Ndipo Paulo akasimama katikati ya Areopago akasema, “Enyi watu wa Athene! Ninaona kwamba katika kila jambo ninyi ni watu wa dini sana.
23Kwa kuwa nilipokuwa nikitembea mjini na kuangalia kwa bidii vitu vyenu vya kuabudiwa, niliona huko madhabahu moja iliyoandikwa: Kwa Mungu Asiyejulikana. Basi sasa kile ambacho mmekuwa mkikiabudu kama kisichojulikana, ndicho ninachowahubiria.
24“Mungu aliyeumba dunia na vyote vilivyomo ndani yake, yeye ndiye Bwana wa mbingu na nchi, hakai katika mahekalu yaliyojengwa kwa mikono ya wanadamu.
25Wala hatumikiwi na mikono ya wanadamu kana kwamba anahitaji chochote, kwa sababu yeye mwenyewe ndiye awapaye watu wote uhai na pumzi na vitu vyote.
26Kutoka kwa mtu mmoja, yeye aliumba mataifa yote ya wanadamu ili waikalie dunia yote, naye akaweka nyakati za kuishi.
27Mungu alifanya hivyo ili wanadamu wamtafute na huenda wakamfikia ingawa kwa kupapasapapasa ijapokuwa kwa kweli hakai mbali na kila mmoja wetu.
28‘Kwa kuwa katika yeye tunaishi, tunatembea na kuwa na uzima wetu.’ Kama baadhi ya watunga mashairi wenu walivyosema, ‘Sisi ni watoto wake.’
29“Kwa kuwa sisi ni watoto wa Mungu, haitupasi kudhani kuwa uungu ni kama sanamu ya dhahabu au ya fedha au ya jiwe, mfano uliotengenezwa kwa ubunifu na ustadi wa mwanadamu.
30Zamani wakati wa ujinga, Mungu alijifanya kama haoni, lakini sasa anawaamuru watu wote kila mahali watubu.
31Kwa kuwa ameweka siku ambayo atauhukumu ulimwengu kwa haki akimtumia mtu aliyemchagua. Amewahakikishia watu wote mambo haya kwa kumfufua Kristo kutoka kwa wafu.”
32Waliposikia habari za ufufuo wa wafu, baadhi yao wakadhihaki, lakini wengine wakasema, “Tunataka kukusikia tena ukizungumza juu ya jambo hili.”
33Kwa hiyo Paulo akaondoka katikati yao.
34Lakini baadhi yao wakaungana naye wakaamini. Kati yao alikuwepo Dionisio, Mwareopago na mwanamke mmoja aliyeitwa Damari na wengine wengi.