1Bwana akamwambia Mose,
2“Waagize Waisraeli wakuletee mafuta safi ya zeituni yaliyokamuliwa kwa ajili ya mwanga ili taa ziwe zinawaka daima.
3Nje ya pazia la Ushuhuda ndani ya Hema la Kukutania, Aroni ataziwasha taa mbele za Bwana kuanzia jioni hadi asubuhi bila kuzima. Hili litakuwa agizo la kudumu kwa vizazi vijavyo.
4Taa zilizo juu ya kinara cha dhahabu safi mbele za Bwana lazima zihudumiwe daima.
5“Chukua unga laini, uoke mikate kumi na miwili, ukitumia sehemu mbili za kumi za efa24:5 Sehemu mbili za kumi za efa ni sawa na kilo mbili. za unga kwa kila mkate.
6Iweke katika mistari miwili, kila mstari mikate sita, uiweke mbele za Bwana juu ya meza iliyotengenezwa kwa dhahabu safi.
7Kando ya kila mstari, weka uvumba safi kama sehemu ya kumbukumbu ili kuwakilisha mikate kuwa sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa kuteketezwa kwa moto.
8Mikate hii itawekwa mbele za Bwana kila wakati, Sabato baada ya Sabato, kwa niaba ya Waisraeli, kuwa Agano la kudumu.
9Hii ni mali ya Aroni na wanawe, watakaoila katika mahali patakatifu, kwa sababu ni sehemu takatifu sana ya fungu lao la kawaida la sadaka iliyotolewa kwa Bwana kwa kuteketezwa kwa moto.”
10Basi mwana wa mama Mwisraeli na baba Mmisri alikwenda miongoni mwa Waisraeli, nayo mapigano yakatokea ndani ya kambi kati yake na Mwisraeli.
11Huyu mwana wa mwanamke Mwisraeli akalikufuru Jina la Bwana kwa kulaani; kwa hiyo wakamleta kwa Mose. (Jina la mama yake aliitwa Shelomithi binti wa Dibri, wa kabila la Dani.)
12Nao wakamweka mahabusu mpaka mapenzi ya Bwana yawe wazi kwao.
13Ndipo Bwana akamwambia Mose:
14“Mchukue huyo aliyekufuru nje ya kambi. Wale wote waliomsikia akikufuru wataweka mikono juu ya kichwa chake, kisha kusanyiko lote litampiga mawe.
15Waambie Waisraeli: ‘Ikiwa mtu yeyote atamlaani Mungu wake, atakuwa na hatia kwa uovu wake;
16yeyote atakayekufuru Jina la Bwana ni lazima auawe. Kusanyiko lote litampiga kwa mawe. Iwe ni mgeni au mzawa, atakapolikufuru Jina la Bwana, ni lazima auawe.
17“ ‘Kama mtu yeyote atamuua mtu mwingine, ni lazima auawe.
18Mtu yeyote auaye mnyama wa mtu mwingine lazima afidie, uhai kwa uhai.
19Ikiwa mtu yeyote atamjeruhi jirani yake, chochote alichomtenda naye atatendewa:
20iwapo amemvunja mfupa atavunjwa mfupa, jicho kwa jicho, jino kwa jino. Kama alivyomjeruhi mwenzake, vivyo hivyo ndivyo atakavyojeruhiwa.
21Yeyote auaye mnyama wa mtu lazima alipe fidia, lakini yeyote auaye mtu, lazima auawe.
22Mtakuwa na sheria iyo hiyo kwa mgeni na kwa mzawa. Mimi ndimi Bwana Mungu wenu.’ ”
23Kisha Mose akasema na Waisraeli, nao wakamchukua yule aliyekufuru nje ya kambi na kumpiga mawe. Waisraeli wakafanya kama Bwana alivyomwagiza Mose.