1Wakati huu Sikukuu ya Mikate Isiyotiwa Chachu, iitwayo Pasaka, ilikuwa imekaribia.
2Viongozi wa makuhani na walimu wa sheria walikuwa wanatafuta njia ya kumuua Yesu, kwa sababu waliwaogopa watu.
3Shetani akamwingia Yuda, aliyeitwa Iskariote, mmoja wa wale Kumi na Wawili.
4Yuda akaenda kwa viongozi wa makuhani na kwa maafisa wa walinzi wa Hekalu, akazungumza nao jinsi ambavyo angeweza kumsaliti Yesu.
5Wakafurahi na wakakubaliana kumpa fedha.
6Naye akakubali, akaanza kutafuta wakati uliofaa wa kumsaliti Yesu kwao, wakati ambapo hakuna umati wa watu.
7Basi ikawadia siku ya Mikate Isiyotiwa Chachu, siku ambayo mwana-kondoo wa Pasaka huchinjwa.
8Hivyo Yesu akawatuma Petro na Yohana, akisema, “Nendeni mkatuandalie chakula cha Pasaka ili tuweze kuila.”
9Wakamuuliza, “Unataka tukuandalie wapi?”
10Yesu akawaambia, “Tazameni, mtakapokuwa mkiingia mjini, mtakutana na mwanaume amebeba mtungi wa maji. Mfuateni mpaka kwenye nyumba atakayoingia.
11Nanyi mwambieni mwenye nyumba, ‘Mwalimu anauliza: Kiko wapi chumba cha wageni, ambamo mimi na wanafunzi wangu tutakula Pasaka?’
12Atawaonyesha chumba kikubwa ghorofani, kikiwa kimepambwa vizuri. Andaeni humo.”
13Wakaenda, nao wakakuta kila kitu kama Yesu alivyowaambia. Hivyo wakaiandaa Pasaka.
14Wakati ulipowadia, Yesu akaketi mezani pamoja na wale mitume wake.
15Kisha akawaambia, “Nimetamani sana kuila Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu.
16Kwa maana, nawaambia, sitaila tena Pasaka mpaka itakapotimizwa katika Ufalme wa Mungu.”
17Akiisha kukichukua kikombe, akashukuru, akasema, “Chukueni hiki mnywe wote.
18Kwa maana nawaambia tangu sasa sitakunywa tena katika uzao wa mzabibu, hadi Ufalme wa Mungu utakapokuja.”
19Kisha akachukua mkate, akashukuru, akaumega, na kuwapa, akisema, “Huu ni mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu. Fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu.”
20Vivyo hivyo baada ya kula, akakitwaa kikombe, akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, imwagikayo kwa ajili yenu.
21Lakini mkono wake huyo atakayenisaliti uko hapa mezani pamoja nami.
22Mwana wa Adamu anaenda zake kama ilivyokusudiwa. Lakini ole wake mtu huyo amsalitiye.”
23Wakaanza kuulizana wenyewe ni nani miongoni mwao angeweza kufanya jambo hilo.
24Pia yakazuka mabishano katikati ya wanafunzi kwamba ni nani aliyeonekana kuwa mkuu kuliko wote miongoni mwao.
25Yesu akawaambia, “Wafalme na watu wa Mataifa huwatawala watu kwa nguvu. Nao wenye mamlaka juu yao hujiita ‘Wafadhili.’
26Lakini ninyi msifanane nao. Bali yeye aliye mkuu kuliko wote miongoni mwenu, inampasa kuwa kama yeye aliye mdogo wa wote, naye atawalaye na awe kama yeye ahudumuye.
27Kwani ni nani aliye mkuu? Ni yule aketiye mezani au ni yule ahudumuye? Si ni yule aliyekaa mezani? Lakini mimi niko miongoni mwenu kama yule ahudumuye.
28Ninyi mmekuwa pamoja nami katika majaribu yangu.
29Nami kama Baba yangu alivyonipa ufalme, kadhalika mimi nami ninawapa ninyi,
30ili mpate kula na kunywa mezani pangu katika karamu ya ufalme wangu, na kukaa katika viti vya enzi, mkihukumu makabila kumi na mawili ya Israeli.”
31Yesu akasema, “Simoni, Simoni, sikiliza, Shetani ameomba kuwapepeta ninyi wote kama ngano.
32Lakini nimekuombea wewe Simoni ili imani yako isishindwe, nawe ukiisha kunirudia, uwaimarishe ndugu zako.”
33Petro akajibu, “Bwana, niko tayari kwenda pamoja nawe gerezani na hata kifoni.”
34Yesu akamjibu, “Ninakuambia Petro, kabla jogoo hajawika usiku wa leo, utakana mara tatu kwamba hunijui mimi.”
35Kisha Yesu akawauliza, “Nilipowatuma bila mfuko, wala mkoba, wala viatu, mlipungukiwa na kitu chochote?”
36Akawaambia, “Lakini sasa, aliye na mfuko na auchukue, na aliye na mkoba vivyo hivyo. Naye asiye na upanga, auze joho lake anunue mmoja.
37Kwa sababu, nawaambia, andiko hili lazima litimizwe juu yangu, kwamba, ‘Alihesabiwa pamoja na wakosaji’; kwa kweli yaliyoandikwa kunihusu mimi hayana budi kutimizwa.”
38Wanafunzi wake wakamwambia, “Bwana, tazama hapa kuna panga mbili.”
39Yesu akatoka, akaenda kwenye Mlima wa Mizeituni kama ilivyokuwa kawaida yake, nao wanafunzi wake wakamfuata.
40Walipofika huko, akawaambia wanafunzi wake, “Ombeni, msije mkaingia majaribuni.”
41Akajitenga nao kama umbali wa kutupa jiwe, akapiga magoti, akaomba
42akisema, “Baba, kama ni mapenzi yako, niondolee kikombe hiki. Lakini si kama nipendavyo, bali mapenzi yako yatendeke.”
43Malaika kutoka mbinguni akamtokea, akamtia nguvu.
44Naye akiwa katika maumivu makuu, akaomba kwa bidii, nalo jasho lake likawa kama matone ya damu yakidondoka ardhini.
45Baada ya kuomba, akawarudia wanafunzi wake akawakuta wamelala, wakiwa wamechoka kutokana na huzuni.
46Naye akawauliza, “Mbona mmelala? Amkeni, mwombe ili msije mkaingia majaribuni.”
47Yesu alipokuwa bado anazungumza, umati mkubwa wa watu ukaja. Uliongozwa na Yuda, ambaye alikuwa mmoja wa wale wanafunzi Kumi na Wawili. Akamkaribia Yesu ili ambusu.
48Lakini Yesu akamwambia, “Yuda, je, unamsaliti Mwana wa Adamu kwa busu?”
49Wafuasi wa Yesu walipoona yale yaliyokuwa yanakaribia kutokea, wakasema, “Bwana, tuwakatekate kwa panga zetu?”
50Mmoja wao akampiga mtumishi wa kuhani mkuu kwa upanga, akamkata sikio la kuume.
51Lakini Yesu akasema, “Acheni!” Akaligusa lile sikio la yule mtu na kumponya.
52Kisha Yesu akawaambia wale viongozi wa makuhani, maafisa wa walinzi wa Hekalu, pamoja na wazee waliokuwa wamekuja kumkamata, “Mmekuja na panga na marungu, kana kwamba mimi ni mnyangʼanyi?
53Siku kwa siku nilikuwa pamoja nanyi Hekaluni lakini hamkunikamata. Lakini hii ni saa yenu, wakati giza linatawala!”
54Kisha wakamkamata Yesu, wakamchukua, wakaenda naye mpaka nyumbani kwa kuhani mkuu. Lakini Petro akafuata kwa mbali.
55Walipokwisha kuwasha moto katikati ya ua na kuketi pamoja, Petro naye akaketi pamoja nao.
56Mtumishi mmoja wa kike akamwona kwa mwanga wa moto akiwa ameketi pale. Akamtazama sana, akasema, “Huyu mtu pia alikuwa pamoja na Yesu!”
57Lakini Petro akakana, akasema, “Ewe mwanamke, hata simjui!”
58Baadaye kidogo, mtu mwingine alimwona Petro akasema, “Wewe pia ni mmoja wao!” Petro akajibu, “Wewe mtu, mimi sio mmoja wao!”
59Baada ya muda wa kama saa moja hivi, mtu mwingine akazidi kusisitiza, “Kwa hakika huyu mtu naye alikuwa pamoja na Yesu, kwa maana yeye pia ni Mgalilaya.”
60Petro akajibu, “Wewe mtu, mimi sijui unalosema!” Wakati huo huo, akiwa bado anazungumza, jogoo akawika.
61Naye Bwana akageuka, akamtazama Petro. Ndipo Petro akakumbuka lile neno ambalo Bwana alimwambia: “Kabla jogoo hajawika leo, utanikana mara tatu.”
62Naye akaenda nje, akalia kwa majonzi.
63Watu waliokuwa wanamlinda Yesu wakaanza kumdhihaki na kumpiga.
64Wakamfunga kitambaa machoni na kumuuliza, “Tabiri! Tuambie ni nani aliyekupiga?”
65Wakaendelea kumtukana kwa matusi mengi.
66Kulipopambazuka, baraza la wazee wa watu,22:66 Baraza la wazee hapa ina maana ya Sanhedrin ambalo lilikuwa ndilo Baraza la juu kabisa la utawala wa Kiyahudi, lililoundwa na wazee 70 pamoja na kuhani mkuu. yaani viongozi wa makuhani na walimu wa sheria, wakakutana pamoja, naye Yesu akaletwa mbele yao.
67Wakamwambia, “Kama wewe ndiye Kristo,22:67 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta. tuambie.”
68Nami nikiwauliza swali, hamtanijibu.
69Lakini kuanzia sasa, Mwana wa Adamu ataketi mkono wa kuume wa Mungu Mwenye Nguvu.”
70Wote wakauliza, “Wewe basi ndiwe Mwana wa Mungu?”
71Kisha wakasema, “Tuna haja gani tena ya ushahidi zaidi? Tumesikia wenyewe kutoka kinywani mwake.”