We Believe JesusFé, Esperança e Nova Vida

Yohana 7

Biblica® Toleo Wazi la Neno: Biblia Takatifu™ · suaíli

← Yohana 6 Yohana Yohana 8 →

1Baada ya mambo haya, Yesu alikwenda sehemu mbalimbali za Galilaya. Hakutaka kwenda Uyahudi kwa sababu Wayahudi huko walitaka kumuua.

2Sikukuu ya Vibanda ya Wayahudi ilikuwa imekaribia.

3Hivyo ndugu zake Yesu wakamwambia, “Ondoka hapa uende Uyahudi ili wanafunzi Wako wapate kuona miujiza unayofanya.

4Mtu anayetaka kujulikana hafanyi mambo yake kwa siri. Kama unafanya mambo haya, jionyeshe kwa ulimwengu.”

5Hata ndugu zake mwenyewe hawakumwamini.

6Yesu akawaambia, “Wakati wangu bado haujawadia, lakini wakati wenu upo siku zote.

7Ulimwengu hauwezi kuwachukia ninyi, lakini unanichukia mimi kwa sababu ninawashuhudia kwamba matendo yao ni maovu.

8Ninyi nendeni kwenye Sikukuu, lakini mimi sitahudhuria Sikukuu hii kwa sababu wakati wangu haujawadia.”

9Akiisha kusema hayo, akabaki Galilaya.

10Lakini ndugu zake walipokwisha kuondoka kwenda kwenye Sikukuu, yeye pia alikwenda lakini kwa siri.

11Wayahudi walikuwa wakimtafuta huko kwenye Sikukuu na kuulizana, “Yuko wapi huyu mtu?”

12Kulikuwa na minongʼono iliyoenea kumhusu Yesu katika umati wa watu, wakati wengine wakisema, “Ni mtu mwema.”

13Lakini hakuna mtu yeyote aliyemsema waziwazi kumhusu kwa sababu ya kuwaogopa Wayahudi.

14Ilipokaribia katikati ya Sikukuu, Yesu alipanda kwenda Hekaluni na kuanza kufundisha.

15Wayahudi wakastaajabia mafundisho yake wakasema, “Mtu huyu amepataje kujua mambo haya bila kufundishwa?”

16Ndipo Yesu akawajibu, “Mafundisho yangu si yangu mwenyewe, bali yanatoka kwake yeye aliyenituma.

17Mtu yeyote akipenda kufanya mapenzi ya Mungu, atajua kama mafundisho yangu yanatoka kwa Mungu au ninasema kwa ajili yangu mwenyewe.

18Wale wanenao kwa ajili yao wenyewe hufanya hivyo kwa kutaka utukufu wao wenyewe. Lakini yeye atafutaye utukufu wa yule aliyemtuma ni wa kweli, wala hakuna uongo ndani yake.

19Je, Mose hakuwapa ninyi sheria? Lakini hakuna hata mmoja wenu anayeishika hiyo sheria. Kwa nini mnataka kuniua?”

20Ule umati wa watu ukamjibu, “Wewe una pepo mchafu! Ni nani anayetaka kukuua?”

21Yesu akawajibu, “Nimefanya muujiza mmoja na nyote mkastaajabu.

22Lakini kwa kuwa Mose aliwaamuru tohara (ingawa kwa kweli haikutoka kwa Mose bali kwa baba zenu wakuu), mnamtahiri mtoto hata siku ya Sabato.

23Ikiwa mtoto aweza kutahiriwa siku ya Sabato kusudi sheria ya Mose isivunjwe, kwa nini mnanikasirikia kwa kumponya mtu mwili wake wote siku ya Sabato?

24Acheni kuhukumu mambo kwa jinsi mnavyoona tu, bali hukumuni kwa haki.”

25Ndipo baadhi ya watu wa Yerusalemu wakawa wanasema, “Tazameni, huyu si yule mtu wanayetaka kumuua?

26Mbona yuko hapa anazungumza hadharani na wala hawamwambii neno lolote? Je, inawezekana viongozi wanafahamu kuwa huyu ndiye Kristo?7:26 Kristo maana yake ni Masiya, yaani Aliyetiwa mafuta.

27Tunafahamu huyu mtu anakotoka, lakini Kristo atakapokuja, hakuna yeyote atakayejua atokako.”

28Ndipo Yesu, akaendelea kufundisha Hekaluni, akisema, “Ninyi mnanifahamu na kujua nitokako. Mimi sikuja kwa ajili yangu mwenyewe, bali yeye aliyenituma ni wa kweli na ninyi hammjui.

29Mimi namjua kwa kuwa nimetoka kwake, naye ndiye alinituma.”

30Ndipo wakatafuta kumkamata, lakini hakuna mtu yeyote aliyethubutu kumshika kwa sababu saa yake ilikuwa bado haijawadia.

31Nao watu wengi wakamwamini, wakasema, “Je, Kristo atakapokuja, atafanya miujiza mikuu zaidi kuliko aliyoifanya mtu huyu?”

32Mafarisayo wakasikia watu wakinongʼona mambo kama hayo kuhusu Yesu, ndipo wao pamoja na viongozi wa makuhani wakatuma walinzi wa Hekalu waende kumkamata.

33Yesu akasema, “Mimi bado niko pamoja nanyi kwa kitambo kidogo, kisha nitarudi kwake yeye aliyenituma.

34Mtanitafuta lakini hamtaniona, nami niliko ninyi hamwezi kuja.”

35Wayahudi wakaulizana wao kwa wao, “Huyu mtu anataka kwenda wapi ambako hatuwezi kumfuata? Je, anataka kwenda kwa Wayunani ambako baadhi ya watu wetu wametawanyikia, akawafundishe Wayunani?

36Yeye ana maana gani anaposema, ‘Mtanitafuta lakini hamtaniona,’ na, ‘nami niliko ninyi hamwezi kuja’?”

37Siku ile ya mwisho ya Sikukuu, siku ile kuu, wakati Yesu akiwa amesimama huko, akapaza sauti yake akasema, “Kama mtu yeyote anaona kiu na aje kwangu anywe.

38Yeyote aniaminiye mimi, kama Maandiko yasemavyo, vijito vya maji ya uzima vitatiririka ndani mwake.”

39Yesu aliposema haya alimaanisha Roho Mtakatifu ambaye wote waliomwamini wangempokea, kwani mpaka wakati huo, Roho alikuwa hajatolewa, kwa kuwa Yesu alikuwa bado hajatukuzwa.

40Waliposikia maneno hayo, baadhi ya watu miongoni mwa ule umati wakasema, “Hakika huyu ndiye yule Nabii.”

41Wengine wakasema, “Huyu ndiye Kristo!”

42Je, Maandiko hayasemi kwamba Kristo atakuja kutoka jamaa ya Daudi na kutoka Bethlehemu, mji alioishi Daudi?”

43Kwa hiyo watu wakagawanyika kwa ajili ya Yesu.

44Baadhi yao walitaka kumkamata, lakini hakuna aliyethubutu kumgusa.

45Hatimaye wale walinzi wa Hekalu wakarudi kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo waliokuwa wamewatuma ili kumkamata Yesu, wakaulizwa, “Mbona hamkumkamata?”

46Wale walinzi wakajibu, “Kamwe hajanena mtu yeyote kama yeye anenavyo.”

47Mafarisayo wakajibu, “Je, nanyi pia mmedanganyika?

48Je, kuna kiongozi yeyote au mmoja wa Mafarisayo ambaye amemwamini?

49Lakini huu umati wa watu wasiojua Sheria ya Mose, wamelaaniwa.”

50Ndipo Nikodemo, yule aliyekuwa amemwendea Yesu siku moja usiku, ambaye alikuwa mmoja wao akauliza,

51“Je, sheria zetu zinaturuhusu kumhukumu mtu kabla ya kumsikiliza na kufahamu alilotenda?”

52Wakamjibu, “Je, wewe pia unatoka Galilaya? Chunguza nawe utaona kwamba hakuna nabii atokae Galilaya!” [

53Kisha wakaondoka, kila mtu akarudi nyumbani kwake.

← Yohana 6 Yohana Yohana 8 →