1Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu, pamoja na Timotheo ndugu yetu:
2kwa dada yetu mpendwa Afia, kwa Arkipo askari mwenzetu na kwa kanisa lile likutanalo nyumbani mwako:
3Neema iwe nanyi na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.
4Siku zote ninamshukuru Mungu ninapokukumbuka katika maombi yangu,
5kwa sababu ninasikia juu ya imani yako katika Bwana Yesu na upendo wako kwa watakatifu wote.
6Naomba utiwe nguvu katika kuishuhudia imani yako, ili upate kuwa na ufahamu mkamilifu juu ya kila kitu chema tulicho nacho ndani ya Kristo.
7Upendo wako umenifurahisha mno na kunitia moyo, kwa sababu wewe ndugu, umeiburudisha mioyo ya watakatifu.
8Hata hivyo, ingawa katika Kristo ningeweza kuwa na ujasiri na kukuagiza yale yakupasayo kutenda,
9lakini ninakuomba kwa upendo, mimi Paulo, mzee na pia sasa nikiwa mfungwa wa Kristo Yesu,
10nakuomba kwa ajili ya mwanangu Onesimo,1:10 Onesimo maana yake ni Wa manufaa. aliyefanyika mwanangu nilipokuwa kwenye minyororo.
11Mwanzoni alikuwa hakufai, lakini sasa anakufaa sana wewe na mimi pia.
12Namtuma kwako, yeye aliye moyo wangu hasa.
13Ningependa nikae naye ili ashike nafasi yako ya kunisaidia wakati huu nikiwa kifungoni kwa ajili ya Injili.
14Lakini sikutaka kufanya lolote bila idhini yako, ili wema wowote uufanyao usiwe wa lazima, bali wa hiari.
15Huenda sababu ya yeye kutengwa nawe kwa kitambo kidogo ni ili uwe naye daima.
16Si kama mtumwa, bali bora kuliko mtumwa, kama ndugu mpendwa. Yeye ni mpendwa sana kwangu na hata kwako zaidi, yeye kama mwanadamu na kama ndugu katika Bwana.
17Hivyo kama unanihesabu mimi kuwa mshirika wako, mkaribishe kama vile ungenikaribisha mimi mwenyewe.
18Kama amekukosea lolote au kama unamdai chochote, nidai mimi.
19Ni mimi Paulo, ninayeandika waraka huu kwa mkono wangu mwenyewe. Nitakulipa. Sitaji kwamba nakudai hata nafsi yako.
20Ndugu yangu, natamani nipate faida kwako katika Bwana, uuburudishe moyo wangu katika Kristo.
21Nikiwa na hakika ya utii wako, nakuandikia, nikijua kwamba utafanya hata zaidi ya yale ninayokuomba.
22Jambo moja zaidi: Niandalie chumba cha wageni, kwa kuwa nataraji kurudishwa kwenu kama jibu la maombi yenu.
23Epafra, aliye mfungwa mwenzangu katika Kristo Yesu, anakusalimu.
24Vivyo hivyo Marko, Aristarko, Dema na Luka, watendakazi wenzangu wanakusalimu.
25Neema ya Bwana Yesu Kristo iwe pamoja na roho zenu. Amen.