We Believe JesusFé, Esperança e Nova Vida

Kutoka 8

Biblica® Toleo Wazi la Neno: Biblia Takatifu™ · suaíli

← Kutoka 7 Kutoka Kutoka 9 →

1Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao ukamwambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu.

2Kama ukikataa kuwaruhusu kuondoka, basi nitaipiga nchi yako yote kwa kuwaletea vyura.

3Mto Naili utafurika vyura. Watakuja kwenye jumba lako la kifalme na katika chumba chako cha kulala na kitandani mwako, katika nyumba za maafisa wako na kwa watu wako, vyura hao wataingia katika meko yenu na kwenye vyombo vya kukandia unga.

4Vyura watapanda juu yako, juu ya watu wako na maafisa wako wote.’ ”

5Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Mwambie Aroni, ‘Nyoosha mkono wako ukiwa na ile fimbo yako juu ya vijito, mifereji na madimbwi, fanya vyura waje juu ya nchi ya Misri.’ ”

6Ndipo Aroni akaunyoosha mkono wake juu ya maji ya Misri, nao vyura wakatokea na kuifunika nchi.

7Lakini waganga wakafanya vivyo hivyo kwa siri ya uganga wao, nao pia wakafanya vyura kuja juu ya nchi ya Misri.

8Ndipo Farao akamwita Mose na Aroni na kusema, “Mwombeni Bwana awaondoe vyura kutoka kwangu na kwa watu wangu, nami nitawaachia watu wenu waende kumtolea Bwana dhabihu.”

9Mose akamwambia Farao, “Ninakupa heshima ya kuamua ni wakati gani wa kukuombea wewe, maafisa wako na watu wako ili kwamba vyura watoke kwenu na kwenye nyumba zenu. Isipokuwa wale walio katika Mto Naili.”

10Farao akasema, “Kesho.”

11Vyura wataondoka kwako na katika nyumba zako, kwa maafisa wako na kwa watu wako, ila watabakia katika Mto Naili tu.”

12Baada ya Mose na Aroni kuondoka kwa Farao, Mose akamlilia Bwana kuhusu vyura aliokuwa amewaleta kwa Farao.

13Naye Bwana akafanya lile Mose alilomwomba. Vyura wakafia ndani ya nyumba, viwanjani na mashambani.

14Wakayakusanya malundo, nchi nzima ikanuka.

15Lakini Farao alipoona pametokea nafuu, akaushupaza moyo wake na hakuwasikiliza Mose na Aroni, kama vile Bwana alivyokuwa amesema.

16Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Mwambie Aroni, ‘Nyoosha fimbo yako uyapige mavumbi ya ardhi,’ nayo nchi yote ya Misri mavumbi yatakuwa viroboto.”

17Wakafanya hivyo, Aroni aliponyoosha mkono wake wenye fimbo na kuyapiga mavumbi ya nchi, viroboto wakawajia watu na wanyama. Mavumbi yote katika nchi ya Misri yakawa viroboto.

18Lakini waganga walipojaribu kutengeneza viroboto kwa siri ya uganga wao, hawakuweza. Nao viroboto walikuwa juu ya watu na wanyama.

19Waganga wale wakamwambia Farao, “Hiki ni kidole cha Mungu.” Lakini moyo wa Farao ukawa mgumu naye hakuwasikiliza, kama vile Bwana alivyosema.

20Kisha Bwana akamwambia Mose, “Amka mapema asubuhi na usimame mbele ya Farao wakati anapokwenda mtoni nawe umwambie, ‘Hili ndilo Bwana asemalo: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu.

21Kama hutawaachia watu wangu waondoke nitakupelekea makundi ya mainzi juu yako, kwa maafisa wako, kwa watu wako na kwenye nyumba zenu. Nyumba za Wamisri zitajazwa mainzi, hata na ardhi yote ya Misri.

22“ ‘Lakini siku ile nitafanya kitu tofauti katika nchi ya Gosheni, ambapo watu wangu wanaishi, hapatakuwepo na makundi ya mainzi, ili mpate kujua kwamba Mimi, Bwana, niko katika nchi hii.

23Nitaweka tofauti kati ya watu wangu na watu wenu. Ishara hii ya ajabu itatokea kesho.’ ”

24Naye Bwana akafanya hivyo. Makundi makubwa ya mainzi yalimiminika katika jumba la kifalme la Farao na katika nyumba za maafisa wake, pia nchi yote ya Misri ikaharibiwa na mainzi.

25Ndipo Farao akamwita Mose na Aroni na kuwaambia, “Nendeni mkamtolee Mungu wenu dhabihu katika nchi hii.”

26Lakini Mose akamwambia, “Hilo halitakuwa sawa. Dhabihu tutakazomtolea Bwana Mungu wetu zitakuwa chukizo kwa Wamisri. Kama tukitoa dhabihu ambazo ni chukizo mbele yao, je, hawatatupiga mawe?

27Ni lazima twende mwendo wa siku tatu mpaka tufike jangwani ili tumtolee Bwana Mungu wetu dhabihu, kama alivyotuagiza.”

28Farao akamwambia, “Nitawaruhusu mwende kumtolea Bwana Mungu wenu dhabihu huko jangwani, lakini hamna ruhusa kwenda mbali sana. Sasa mniombee.”

29Mose akajibu, “Mara tu nitakapoondoka, nitamwomba Bwana na kesho mainzi yataondoka kwa Farao, kwa maafisa wake na kwa watu wake. Hakikisha tu kwamba Farao hatatenda kwa udanganyifu tena kwa kutokuwaachia watu waende kumtolea Bwana dhabihu.”

30Ndipo Mose akamwacha Farao na kumwomba Bwana,

31naye Bwana akafanya lile Mose alilomwomba. Mainzi yakaondoka kwa Farao, kwa maafisa wake na kwa watu wake, wala hakuna hata inzi aliyebakia.

32Lakini wakati huu pia Farao akaushupaza moyo wake, wala hakuwaruhusu Waisraeli waondoke.

← Kutoka 7 Kutoka Kutoka 9 →