1Mose akamjibu, “Itakuwaje kama hawataniamini au kunisikiliza, waseme, ‘Bwana hakukutokea’?”
2Ndipo Bwana akamwambia, “Ni nini hicho kilicho mkononi mwako?”
3Bwana akasema, “Itupe chini.”
4Kisha Bwana akamwambia, “Nyoosha mkono wako umkamate mkiani.” Basi Mose akanyoosha mkono akamkamata yule nyoka, naye akabadilika tena kuwa fimbo mkononi mwake.
5Bwana akasema, “Hivi ndivyo Waisraeli watakavyoamini kuwa Bwana, Mungu wa baba zao, Mungu wa Abrahamu, Mungu wa Isaki, na Mungu wa Yakobo, amekutokea wewe.”
6Kisha Bwana akamwambia, “Weka mkono wako ndani ya joho lako.” Basi Mose akaweka mkono wake ndani ya joho lake, naye alipoutoa, ulikuwa na ukoma, mweupe kama theluji.
7Mungu akamwambia, “Sasa urudishe tena huo mkono ndani ya joho lako.” Basi Mose akaurudisha mkono wake ndani ya joho lake na alipoutoa, ulikuwa mzima, kama sehemu zingine za mwili wake.
8Ndipo Bwana akamwambia, “Kama hawatakuamini wewe, au kutojali ishara ya kwanza, wataamini ishara ya pili.
9Lakini kama hawataamini ishara hizi mbili au hawatawasikiliza ninyi, chukua kiasi cha maji kutoka Mto Naili uyamimine juu ya ardhi kavu. Maji mtakayotoa mtoni yatakuwa damu juu ya ardhi.”
10Mose akamwambia Bwana, “Ee Bwana, kamwe sijapata kuwa msemaji kwa ufasaha wakati uliopita wala tangu ulipoanza kuzungumza na mtumishi wako. Ulimi wangu ni mzito kuzungumza.”
11Bwana akamwambia, “Ni nani aliyempa mwanadamu kinywa? Ni nani aliyemfanya mtu kuwa kiziwi au bubu? Ni nani anayempa mtu kuona au upofu? Je, si mimi, Bwana?
12Sasa nenda, nitakusaidia kusema, nami nitakufundisha jambo la kusema.”
13Lakini Mose akasema, “Ee Bwana, tafadhali mtume mtu mwingine kufanya kazi hiyo.”
14Ndipo hasira ya Bwana ikawaka dhidi ya Mose, akamwambia, “Vipi kuhusu ndugu yako, Aroni Mlawi? Ninajua yeye anaweza kuzungumza vizuri. Naye yuko tayari njiani kukulaki, na moyo wake utafurahi wakati atakapokuona.
15Utazungumza naye na kuweka maneno kinywani mwake. Nitawasaidia ninyi wawili kusema, nami nitawafundisha jambo la kufanya.
16Aroni ataongea na watu badala yako na itakuwa kwamba yeye amekuwa kinywa chako nawe utakuwa kama Mungu kwake.
17Lakini chukua fimbo hii mkononi mwako ili uweze kuitumia kufanya ishara hizo za ajabu.”
18Kisha Mose akarudi kwa Yethro mkwewe akamwambia, “Niruhusu nirudi kwa watu wangu Misri kuona kama yuko hata mmoja wao ambaye bado anaishi.”
19Basi Bwana alikuwa amemwambia Mose huko Midiani, “Rudi Misri kwa maana watu wote waliotaka kukuua wamekufa.”
20Basi Mose akamchukua mkewe na wanawe, akawapandisha juu ya punda na kuanza safari kurudi Misri. Naye akaichukua ile fimbo ya Mungu mkononi mwake.
21Bwana akamwambia Mose, “Utakaporudi Misri, hakikisha kwamba utafanya mbele ya Farao maajabu yote niliyokupa uwezo wa kuyafanya. Lakini nitafanya moyo wake kuwa mgumu ili kwamba asiwaruhusu watu waende.
22Kisha mwambie Farao, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Israeli ni mwanangu mzaliwa wa kwanza,
23nami nilikuambia, “Ruhusu mwanangu aondoke, ili aweze kuniabudu mimi.” Lakini ukakataa kumruhusu kwenda, basi nitaua mwana wako mzaliwa wa kwanza.’ ”
24Mose alipokuwa mahali pa kulala wageni akiwa njiani kurudi Misri, Bwana akakutana naye, akataka kumuua.
25Lakini Sipora akachukua jiwe gumu, akakata govi la mwanawe na kugusa nalo miguu ya Mose. Sipora akasema, “Hakika wewe ni bwana arusi wa damu kwangu.”
26Sipora alipomwita Mose, “Bwana arusi wa damu,” alikuwa anamaanisha ile tohara. Baada ya hayo Bwana akamwacha.
27Bwana akamwambia Aroni, “Nenda jangwani ukamlaki Mose.” Basi akakutana na Mose kwenye mlima wa Mungu, akambusu.
28Kisha Mose akamwambia Aroni kila kitu Bwana alichomtuma kusema, vilevile habari za ishara na maajabu alizokuwa amemwamuru kufanya.
29Mose na Aroni wakawakusanya wazee wote wa Waisraeli,
30naye Aroni akawaambia kila kitu Bwana alichokuwa amemwambia Mose. Pia akafanya ishara mbele ya watu,
31nao wakaamini. Nao waliposikia kuwa Bwana anajishughulisha nao, na kwamba ameona mateso yao, walisujudu na kuabudu.