1Ndipo Mungu akasema maneno haya yote:
2“Mimi ndimi Bwana Mungu wako, niliyekutoa Misri, kutoka nchi ya utumwa.
3Usiwe na miungu mingine ila mimi.
4Usijitengenezee sanamu katika umbo la kitu chochote kilicho juu mbinguni, au duniani chini, au ndani ya maji.
5Usivisujudie wala kuviabudu; kwa kuwa Mimi, Bwana Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu, ninayewaadhibu watoto kwa ajili ya dhambi za baba zao hadi kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,
6lakini ninaonyesha upendo kwa maelfu ya vizazi vya wale wanipendao na kuzishika amri zangu.
7Usilitaje bure jina la Bwana Mungu wako, kwa kuwa Bwana hataacha kumhesabia hatia yeye alitajaye jina lake bure.
8Ikumbuke siku ya Sabato, uitakase.
9Kwa siku sita utafanya kazi na kutenda shughuli zako zote,
10lakini siku ya saba ni Sabato kwa Bwana Mungu wako. Siku hiyo hutafanya kazi yoyote, wewe, wala mwanao au binti yako, wala mtumishi wako wa kiume au wa kike, wala wanyama wako, wala mgeni aliye ndani ya malango yako.
11Kwa kuwa kwa siku sita, Bwana aliumba mbingu na nchi, bahari na vyote vilivyomo, lakini akapumzika siku ya saba. Kwa hiyo Bwana akaibariki siku ya Sabato na kuifanya takatifu.
12Waheshimu baba yako na mama yako, ili upate kuishi siku nyingi katika nchi anayokupa Bwana Mungu wako.
13Usiue.
14Usizini.
15Usiibe.
16Usimshuhudie jirani yako uongo.
17Usiitamani nyumba ya jirani yako. Usimtamani mke wa jirani yako, wala mtumishi wake wa kiume au wa kike, wala ngʼombe wake au punda wake, wala chochote kile alicho nacho jirani yako.”
18Watu walipoona ngurumo na radi, na kusikia mlio wa tarumbeta, na kuuona mlima katika moshi, walitetemeka kwa woga. Wakasimama mbali
19na wakamwambia Mose, “Sema nasi wewe mwenyewe, nasi tutakusikiliza. Lakini usimwache Mungu aseme nasi, la sivyo tutakufa.”
20Mose akawaambia watu, “Msiogope! Mungu amekuja kuwajaribu, ili kwamba hofu ya Mungu iwakalie, msitende dhambi.”
21Watu wakabaki mbali, wakati Mose alipolisogelea lile giza nene mahali pale Mungu alipokuwa.
22Kisha Bwana akamwambia Mose, “Waambie Waisraeli hivi: ‘Mmejionea wenyewe kwamba nimesema nanyi kutoka mbinguni:
23Msijifanyizie miungu yoyote na kuilinganisha nami, msijitengenezee miungu ya fedha wala miungu ya dhahabu.
24“ ‘Utanitengenezea madhabahu ya udongo, na juu yake utoe sadaka za kuteketezwa kwa moto na sadaka za amani, kondoo zako, mbuzi na ngʼombe zako. Popote nitakapofanya Jina langu liheshimiwe, nitakuja kwenu na kuwabariki.
25Ikiwa unanitengenezea madhabahu ya mawe, usiijenge kwa mawe ya kuchonga, maana mkitumia chombo cha kuchongea mtaitia unajisi.
26Msitumie ngazi kupandia kwenye madhabahu yangu, uchi wako usije ukadhihirika kwa chini.’