We Believe JesusFé, Esperança e Nova Vida

Kumbukumbu 11

Biblica® Toleo Wazi la Neno: Biblia Takatifu™ · suaíli

← Kumbukumbu 10 Kumbukumbu Kumbukumbu 12 →

1Mpende Bwana Mungu wako na kushika masharti yake, amri zake, sheria zake na maagizo yake siku zote.

2Kumbuka hivi leo kwamba sio watoto wako walioona na kujua adhabu ya Bwana Mungu wako: utukufu wake, mkono wake wenye nguvu, mkono wake ulionyooshwa;

3ishara alizozifanya na mambo aliyoyafanya katikati ya Misri, kwa Farao mfalme wa Misri na kwa nchi yake yote;

4lile alilolifanyia jeshi la Wamisri, farasi na magari yake, jinsi alivyowafurikisha na maji ya Bahari ya Shamu walipokuwa wakiwafuatilia ninyi, na jinsi Bwana alivyowaletea angamizo la kudumu juu yao.

5Sio watoto wenu walioyaona yale Mungu aliyowafanyia huko jangwani mpaka mkafika mahali hapa,

6wala lile Mungu alilowafanyia Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu wa kabila la Reubeni, wakati ardhi ilipofungua kinywa chake katikati ya Israeli yote, ikawameza pamoja na walio nyumbani mwao, hema zao na kila kitu kilichokuwa hai ambacho kilikuwa mali yao.

7Bali ilikuwa ni macho yenu wenyewe ambayo yaliyaona mambo haya yote makuu Bwana aliyoyatenda.

8Kwa hiyo fuateni maagizo yote ninayowapa leo, ili mpate kuwa na nguvu za kuingia na kuiteka nchi ile ambayo mnavuka Yordani kuimiliki,

9ili mpate kuishi siku nyingi katika nchi ile ambayo Bwana aliapa kuwapa baba zenu na wazao wao, nchi itiririkayo maziwa na asali.

10Nchi mnayoiingia kuimiliki haifanani na nchi ya Misri mlikotoka ambako mlipanda mbegu yenu na kuinywesha, kama bustani ya mboga.

11Lakini nchi mnayovuka Yordani kuimiliki ni nchi ya milima na mabonde inywayo mvua kutoka mbinguni.

12Ni nchi ambayo Bwana Mungu wenu anaitunza; macho ya Bwana Mungu wenu yanaitazama daima kutoka mwanzo wa mwaka hadi mwisho wa mwaka.

13Hivyo kama mkiyatii maagizo yangu ninayowapa leo kwa uaminifu, yaani kwa kumpenda Bwana Mungu wenu, na kumtumikia kwa moyo wako wote na kwa roho yenu yote,

14ndipo atawanyweshea mvua katika nchi yenu kwa majira yake, mvua ya masika na ya vuli, ili mpate kuvuna nafaka zenu, divai mpya na mafuta.

15Nitawapa majani kwa ajili ya ngʼombe wenu, nanyi mtakula na kushiba.

16Jihadharini, la sivyo mtashawishika kugeuka na kuabudu miungu mingine na kuisujudia.

17Ndipo hasira ya Bwana itawaka dhidi yenu, naye atafunga mbingu ili mvua isinyeshe nayo ardhi haitatoa mazao, nanyi mtaangamia mara katika nchi nzuri ambayo Bwana anawapa.

18Yawekeni haya maneno yangu katika mioyo yenu na akili zenu, yafungeni kama alama juu ya mikono yenu na kwenye paji za nyuso zenu.

19Wafundisheni watoto wenu, yazungumzeni wakati mketipo nyumbani na wakati mtembeapo njiani, wakati mlalapo na wakati mwamkapo.

20Yaandikeni juu ya miimo ya nyumba zenu na juu ya malango yenu,

21ili kwamba siku zenu na siku za watoto wenu zipate kuwa nyingi katika nchi ile Bwana aliyoapa kuwapa baba zenu, kama zilivyo nyingi siku za mbingu juu ya nchi.

22Kama mkishika kwa makini maagizo haya yote ninayowapa kuyafuata, ya kumpenda Bwana Mungu wenu, kuenenda katika njia zake zote na kushikamana naye kwa uthabiti,

23ndipo Bwana atawafukuza mataifa haya yote mbele yako, nawe utawafukuza mataifa yaliyo makubwa na yenye nguvu kukuliko wewe.

24Kila mahali mtakapoweka mguu wenu patakuwa penu: Nchi yenu itaenea kutoka jangwa la Lebanoni, na kutoka mto wa Frati hadi bahari ya magharibi11:24 Yaani Bahari ya Mediterania.

25Hapatakuwa na mtu atakayeweza kusimama dhidi yenu. Bwana Mungu wenu, kama alivyoahidi, ataweka juu ya nchi yote utisho na hofu kwa ajili yenu popote mwendako.

26Tazama, leo ninaweka mbele yenu baraka na laana:

27baraka kama mtatii maagizo ya Bwana Mungu wenu, ambayo ninawapa leo;

28laana kama hamtatii maagizo ya Bwana Mungu wenu na kuacha njia ambayo ninawaamuru leo kwa kufuata miungu mingine, ambayo hamkuijua.

29Wakati Bwana Mungu wenu atakapokuwa amewaleta katika nchi mnayoiingia kuimiliki, mtatangaza baraka kutoka Mlima Gerizimu, na kutangaza laana kutoka Mlima Ebali.

30Kama mnavyofahamu, milima hii ipo ngʼambo ya Yordani, magharibi ya barabara, kuelekea machweo ya jua, karibu na miti mikubwa ya More, katika nchi ya wale Wakanaani wanaoishi Araba, jirani na Gilgali.

31Karibu mvuke ngʼambo ya Yordani kuingia na kuimiliki nchi ambayo Bwana Mungu wenu anawapa. Wakati mtakapokuwa mmeichukua na mnaishi humo,

32hakikisheni kwamba mnatii amri na sheria zote ninazoziweka mbele yenu leo.

← Kumbukumbu 10 Kumbukumbu Kumbukumbu 12 →