1Ninyi mabwana, watendeeni watumwa wenu yaliyo haki na yanayostahili, mkitambua ya kwamba ninyi pia mnaye Bwana mbinguni.
2Dumuni sana katika maombi, mkikesha katika hayo pamoja na kushukuru.
3Pia tuombeeni na sisi ili Mungu atufungulie mlango wa kunena, ili tupate kuitangaza siri ya Kristo, ambayo kwa ajili yake pia mimi nimefungwa.
4Ombeni ili nipate kuitangaza Injili kwa udhahiri kama ipasavyo kunena.
5Enendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati.
6Maneno yenu yawe yamejaa neema siku zote, yanayofaa, ili mjue jinsi iwapasavyo na inavyofaa kumjibu kila mtu.
7Tikiko atawaambia habari zangu zote. Yeye ni ndugu mpendwa, mtendakazi mwaminifu na mtumishi mwenzangu katika Bwana.
8Nimemtuma kwenu kwa madhumuni haya ili mpate kufahamu hali yetu, na pia awatie moyo.
9Anakuja pamoja na Onesimo, ndugu yetu mpendwa na mwaminifu, ambaye ni mmoja wenu. Watawaambia mambo yote yanayotendeka hapa kwetu.
10Aristarko aliye mfungwa pamoja nami anawasalimu, vivyo hivyo Marko, binamu yake Barnaba. (Mmeshapata maagizo yanayomhusu; akija kwenu, mpokeeni.)
11Yesu, yeye aitwaye Yusto, pia anawasalimu. Hawa peke yao ndio Wayahudi miongoni mwa watendakazi wenzangu kwa ajili ya Ufalme wa Mungu, nao wamekuwa faraja kwangu.
12Epafra, ambaye ni mmoja wenu na mtumishi wa Kristo Yesu, anawasalimu. Yeye siku zote anawaombea kwa bidii kwamba msimame imara katika mapenzi yote ya Mungu, mkiwa wakamilifu na thabiti.
13Ninashuhudia kumhusu kwamba anafanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu, na kwa ajili ya ndugu wa Laodikia na wale wa Hierapoli.
14Rafiki yetu mpenzi Luka yule tabibu, pamoja na Dema, wanawasalimu.
15Wasalimuni ndugu wote wa Laodikia, na pia Nimfa, pamoja na kanisa linalokutana katika nyumba yake.
16Baada ya barua hii kusomwa kwenu, hakikisheni kwamba inasomwa pia katika kanisa la Walaodikia. Nanyi pia msome barua inayotoka Laodikia.
17Mwambieni Arkipo hivi: “Hakikisha kuwa unakamilisha ile huduma uliyopokea katika Bwana.”
18Mimi, Paulo, naandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe. Kumbukeni minyororo yangu. Neema iwe nanyi. Amen.