1Ndugu, kuhusu kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo na kukusanyika kwetu pamoja mbele zake, tunawasihi,
2msiyumbishwe kwa urahisi wala msitiwe wasiwasi na roho wala neno au barua inayosemekana kuwa imetoka kwetu, isemayo kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwako.
3Mtu yeyote na asiwadanganye kwa namna yoyote kwa maana siku ile haitakuja mpaka uasi utokee kwanza, na yule mtu wa kuasi adhihirishwe, yule ambaye amehukumiwa kuangamizwa kabisa.
4Yeye atapingana na kujitukuza juu ya kila kitu kiitwacho Mungu au kinachoabudiwa, ili kujiweka juu katika Hekalu la Mungu, akijitangaza mwenyewe kuwa ndiye Mungu.
5Je, hamkumbuki ya kwamba nilipokuwa pamoja nanyi niliwaambia mambo haya?
6Nanyi sasa mnajua kinachomzuia, ili apate kudhihirishwa wakati wake utakapowadia.
7Maana ile nguvu ya siri ya uasi tayari inatenda kazi, lakini yule anayeizuia ataendelea kufanya hivyo mpaka atakapoondolewa.
8Hapo ndipo yule mwasi atafunuliwa, ambaye Bwana Yesu atamteketeza kwa pumzi ya kinywa chake na kumwangamiza kabisa kwa utukufu wa kuja kwake.
9Kuja kwa yule mwasi kutaonekana kana kwamba ni kutenda kazi kwake Shetani ambaye hutumia nguvu zote, ishara, maajabu ya uongo,
10na kila aina ya uovu kwa wale wanaoangamia kwa sababu walikataa kuipenda kweli wapate kuokolewa.
11Kwa sababu hii, Mungu ameruhusu watawaliwe na nguvu ya udanganyifu, ili waendelee kuamini uongo,
12na wahukumiwe wote ambao hawakuiamini ile kweli, bali wamefurahia uovu.
13Lakini imetupasa sisi kumshukuru Mungu daima kwa ajili yenu, ndugu mpendwao na Bwana, kwa sababu Mungu aliwachagua ninyi tangu mwanzo ili mwokolewe kwa kutakaswa na Roho kwa kuiamini kweli.
14Kwa kusudi hili Mungu aliwaita kwa njia ya kuhubiri kwetu Injili, ili mpate kushiriki katika utukufu wa Bwana Yesu Kristo.
15Hivyo basi, ndugu wapendwa, simameni imara na myashike sana yale mafundisho tuliyowapa ikiwa ni kwa maneno ya kinywa au kwa barua.
16Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe na Mungu Baba yetu, aliyetupenda na kwa neema yake akatupatia faraja ya milele na tumaini jema,
17awafariji mioyo yenu na kuwaimarisha katika kila neno na tendo jema.