We Believe JesusFé, Esperança e Nova Vida

2 Samweli 8

Biblica® Toleo Wazi la Neno: Biblia Takatifu™ · suaíli

← 2 Samweli 7 2 Samweli 2 Samweli 9 →

1Baada ya muda, Daudi akawashinda Wafilisti na kuwatiisha, naye akautwaa Metheg-Amma kutoka mikononi mwa Wafilisti.

2Pia Daudi akawashinda Wamoabu. Akawafanya walale chini kwa mstari akawapima kwa urefu wa kamba. Kila alipopima urefu wa hiyo kamba mara mbili hilo kundi waliuawa na alipopima mara ya tatu aliwaacha hai. Kwa hiyo Wamoabu wakawa chini ya Daudi nao wakamletea kodi.

3Zaidi ya hayo, Daudi akapigana na Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba, alipokwenda kurudisha tena utawala wake kwenye eneo la Mto Frati.

4Daudi akateka magari yake ya vita 1,000, askari wapanda farasi 7,000 na askari 20,000 watembeao kwa miguu. Daudi akawakata wale farasi wote wakokotao magari mishipa ya miguu, isipokuwa farasi 100 hakuwakata.

5Waaramu wa Dameski walipokuja kumsaidia Hadadezeri mfalme wa Soba, Daudi akawashambulia na kuwaua 22,000 miongoni mwao.

6Daudi akaweka askari walinzi katika ufalme wa Waaramu huko Dameski, nao Waaramu wakawa watumwa wake na kumlipa ushuru. Bwana akampa Daudi ushindi kote alipokwenda.

7Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizokuwa za maafisa wa Hadadezeri na kuzileta Yerusalemu.

8Kutoka miji ya Beta8:8 Beta ulikuwa mji wa Aramu-Soba ambao uliitwa Teba kwa Kiaramu; pia uliitwa Tibhathi (1Nya 18:8). na Berothai, iliyokuwa miji ya Hadadezeri, Mfalme Daudi akatwaa shaba nyingi sana.

9Tou, mfalme wa Hamathi, aliposikia kwamba Daudi amelishinda jeshi lote la Hadadezeri,

10akamtuma mwanawe Yoramu kwa Mfalme Daudi kumsalimu na kumpongeza kwa ushindi wake katika vita dhidi ya Hadadezeri, kwa kuwa Hadadezeri alikuwa amepigana vita na Tou. Yoramu akamletea Daudi vyombo vya fedha, dhahabu na shaba.

11Mfalme Daudi akaviweka vifaa hivi wakfu kwa Bwana, kama vile alivyokuwa amefanya kwa fedha na dhahabu kutoka kwa mataifa yote aliyokuwa ameyashinda:

12yaani Edomu, Moabu, Waamoni, Wafilisti na Waamaleki. Pia akaweka wakfu nyara alizoteka kutoka kwa Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba.

13Naye Daudi akapata sifa baada ya kurudi kutoka kuwaua Waedomu 18,000 katika Bonde la Chumvi.

14Akaweka kambi za askari walinzi katika Edomu yote, nao Waedomu wakawa chini ya Daudi. Bwana alimpatia Daudi ushindi kila alipokwenda.

15Daudi akatawala Israeli yote, akitenda lililo haki na sawa kwa watu wake wote.

16Yoabu mwana wa Seruya alikuwa jemadari wa jeshi; Yehoshafati mwana wa Ahiludi alikuwa mweka kumbukumbu;

17Sadoki mwana wa Ahitubu na Ahimeleki mwana wa Abiathari walikuwa makuhani; Seraya alikuwa mwandishi;

18Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa msimamizi wa Wakerethi na Wapelethi; nao wana wa Daudi walikuwa washauri wa mfalme.

← 2 Samweli 7 2 Samweli 2 Samweli 9 →