We Believe JesusFé, Esperança e Nova Vida

2 Nyakati 11

Biblica® Toleo Wazi la Neno: Biblia Takatifu™ · suaíli

← 2 Nyakati 10 2 Nyakati 2 Nyakati 12 →

1Ikawa Rehoboamu alipofika Yerusalemu, akakusanya nyumba ya Yuda na ya Benyamini, wanaume wapiganaji 180,000, kufanya vita dhidi ya nyumba ya Israeli na kuurudisha tena ufalme kwa Rehoboamu mwana wa Solomoni.

2Lakini neno hili la Bwana likamjia Shemaya mtu wa Mungu:

3“Mwambie Rehoboamu mwana wa Solomoni mfalme wa Yuda, na Israeli wote walioko Yuda na Benyamini,

4‘Hili ndilo asemalo Bwana: Msipande kupigana dhidi ya ndugu zenu. Nendeni nyumbani, kila mmoja wenu, kwa kuwa hili nimelitenda mimi.’ ” Kwa hiyo wakalitii neno la Bwana na wakaacha kwenda kupigana dhidi ya Yeroboamu.

5Rehoboamu akaishi Yerusalemu akajenga miji yenye ngome katika Yuda:

6Akajenga Bethlehemu, Etamu, Tekoa,

7Beth-Suri, Soko, Adulamu,

8Gathi, Maresha, Zifu,

9Adoraimu, Lakishi, Azeka,

10Sora, Aiyaloni na Hebroni. Hii ndiyo iliyokuwa miji iliyojengewa ngome katika Yuda na Benyamini.

11Akaimarisha ulinzi wake na kuweka majemadari ndani yake, pamoja na ghala za mahitaji ya vyakula, mafuta ya zeituni na divai.

12Akaweka ngao na mikuki katika miji na kuifanya iwe imara sana. Kwa hiyo Yuda na Benyamini zikawa zake.

13Makuhani na Walawi kutoka sehemu zote za Israeli wakawa upande wake.

14Pia Walawi wakaacha maeneo yao ya malisho na mali zao, wakaja Yuda na Yerusalemu kwa sababu Yeroboamu na wanawe walikuwa wamewakataa wasiwe makuhani wa Bwana.

15Naye akawa amechagua makuhani wake mwenyewe kwa ajili ya mahali pa juu pa kuabudia sanamu za mbuzi na za ndama ambazo alikuwa ametengeneza.

16Wale waliotoka katika kila kabila la Israeli ambao walielekeza mioyo yao kumtafuta Bwana, Mungu wa Israeli, wakawafuata Walawi huko Yerusalemu kumtolea Bwana dhabihu, Mungu wa baba zao.

17Wakaimarisha ufalme wa Yuda na kumuunga mkono Rehoboamu mwana wa Solomoni miaka mitatu, wakienenda katika njia za Daudi na Solomoni katika wakati huu.

18Rehoboamu alimwoa Mahalati ambaye alikuwa binti Yeremothi mwana wa Daudi, mamaye alikuwa Abihaili binti Eliabu mwana wa Yese.

19Mahalati alimzalia Rehoboamu wana: Yeushi, Shemaria na Zahamu.

20Kisha akamwoa Maaka binti Absalomu, ambaye alimzalia: Abiya, Atai, Ziza na Shelomithi.

21Rehoboamu akampenda Maaka binti Absalomu zaidi kuliko wakeze wengine na masuria wake. Kwa jumla alikuwa na wake kumi na wanane na masuria sitini, wana ishirini na wanane na binti sitini.

22Rehoboamu akamweka Abiya mwana wa Maaka, kuwa mkuu wa wana wa mfalme miongoni mwa ndugu zake ili amfanye mfalme.

23Akatenda kwa busara, akiwasambaza baadhi ya wanawe katika wilaya zote za Yuda na Benyamini, pamoja na miji yote yenye ngome. Akawapa mahitaji tele na kuwaoza wake wengi.

← 2 Nyakati 10 2 Nyakati 2 Nyakati 12 →