1Siku zile Wafilisti wakakusanya majeshi yao ili kupigana vita dhidi ya Israeli. Akishi akamwambia Daudi, “Lazima ujue kuwa wewe pamoja na watu wako mtafuatana nami kwenda vitani.”
2Daudi akasema, “Ndipo wewe mwenyewe utakapojionea jambo ambalo mtumishi wako anaweza kufanya.”
3Wakati huo Samweli alikuwa amekufa, nao Israeli wote walikuwa wamemwombolezea na kumzika kwenye mji wake mwenyewe huko Rama. Sauli alikuwa amewafukuza waaguzi na wachawi.
4Wafilisti wakakusanyika na kupiga kambi yao huko Shunemu, naye Sauli akawakusanya Waisraeli wote na kupiga kambi yao huko Gilboa.
5Sauli alipoona jeshi la Wafilisti, akaogopa; moyo wake ukajawa na hofu kuu.
6Ndipo Sauli akauliza ushauri kwa Bwana, lakini Bwana hakumjibu kwa ndoto, wala kwa Urimu,28:6 Urimu na Thumimu maana yake ni Nuru na Kweli; vifaa hivi viliwekwa kwenye kifuko cha juu cha kisibau cha kuhani mkuu ili kujua mapenzi ya Mungu kwenye mambo ya kutatanisha. wala kwa njia ya manabii.
7Basi Sauli akawaambia watumishi wake, “Nitafutieni mwanamke mwaguzi ili nimwendee, nipate kuuliza kwake.”
8Hivyo Sauli akajigeuza kwa kuvaa mavazi mengine, naye usiku akiwa amefuatana na watu wawili wakaenda kwa huyo mwanamke. Akamwambia, “Nibashirie kwa uaguzi, unipandishie yule nitakayekutajia.”
9Huyo mwanamke akamwambia, “Wewe unajua lile alilofanya Mfalme Sauli. Amewakatilia mbali waaguzi, wapiga ramli wote na wachawi katika nchi. Mbona umenitegea maisha yangu ili wapate kuniua?”
10Sauli akamwapia huyo mwanamke kwa Jina la Bwana, akasema, “Kwa hakika kama Bwana aishivyo, hutaadhibiwa kwa ajili ya jambo hili.”
11Ndipo yule mwanamke akauliza, “Je unataka nikupandishie nani?”
12Yule mwanamke alipomwona Samweli, alipiga yowe kwa sauti kuu, naye akamuuliza Sauli, “Mbona umenidanganya? Wewe ndiwe Sauli.”
13Mfalme akamwambia, “Usiogope. Unaona nini?”
14Sauli akamuuliza, “Ni mfano wa nini?”
15Samweli akamuuliza Sauli, “Kwa nini unanitaabisha kwa kunipandisha juu?”
16Samweli akamuuliza, “Kwa nini uniulize mimi, maadamu Bwana amekuacha na kuwa adui yako?
17Bwana ametenda lile alilotangulia kusema kupitia kwangu. Bwana ameurarua ufalme kutoka mikononi mwako, naye amempa mmoja wa jirani zako, yaani Daudi.
18Kwa sababu wewe hukumtii Bwana, wala hukumtimizia ghadhabu yake kali juu ya Waamaleki, Bwana amekutendea mambo haya leo.
19Zaidi ya hayo, Bwana atawatia Israeli pamoja na wewe mikononi mwa Wafilisti, na kesho wewe na wanao mtakuwa pamoja nami. Bwana pia atalitia jeshi la Israeli mikononi mwa Wafilisti.”
20Papo hapo Sauli akaanguka chini, akajinyoosha, akiwa amejawa na hofu kwa ajili ya maneno ya Samweli. Nguvu zake zikamwishia kwa maana alikuwa hajala chochote mchana ule wote na usiku.
21Yule mwanamke alipomwendea Sauli na kumwona amepatwa na hofu, akamwambia, “Tazama, mimi mtumishi wako mwanamke nimekutii. Nimeweka maisha yangu hatarini kwa kufanya kile ulichoniagiza nifanye.
22Sasa tafadhali isikilize sauti ya mtumishi wako, uniruhusu nikupatie chakula kidogo ule ili uwe na nguvu za kurejea ulikotoka.”
23Akakataa, akisema, “Mimi sitaki kula.”
24Yule mwanamke alikuwa na ndama aliyenona hapo nyumbani, akamchinja mara moja. Akachukua unga, akaukanda, akatengeneza mkate usio chachu.
25Ndipo akamwandalia meza Sauli pamoja na watu wake, nao wakala. Usiku ule ule wakainuka na kwenda zao.